Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ahadi ya JPM barabara Tanga-Pangani ‘yaiva’

GTE Ahadi ya JPM barabara Tanga-Pangani ‘yaiva’

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

AHADI ya Rais John Magufuli, ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 50 kutoka Tanga mjini hadi Pangani imeanza kutekelezwa, kwa mkandarasi kuanza hatua za awali kuelekea ujenzi kamili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Tanga, Alfred Ndumbaro, alisema mkandarasi kampuni ya China Henan International Cooperation Group Company (Chico) tayari yupo eneo la mradi.

“Mkandarasi yupo katika hatua za ukamilishaji wa kambi kwa ajili ya kuhifadhi vifaa na makazi katika eneo la Tongoni na Marungu.”

“Tumefanikiwa kupata maeneo mawili kwa ajili ya ujenzi wa makambi, ambapo yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyingine za ujenzi,” alisema.

Ndumbaro alisema mkandarasi ameanza kupeleka baadhi ya vifaa vya kazi eneo la ujenzi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kazi kuanza. Hata hivyo, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni ucheleweshaji wa malipo ya fidia kwa wananchi.

“Licha ya changamoto hiyo, lakini tayari mkandarasi ameshaanza usafishaji wa eneo la barabara kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi katika maeneo ambayo hayana changamoto ya fidia,” alisema.

Serikali imetenga Sh bilioni 66.8 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tanga hadi Pangani yenye urefu wa kilomita 50.

Chanzo: habarileo.co.tz