Shule kuu ya Uuguzi na Ukunga ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza imetangaza programu mpya ya kuwadahili wanafunzi wa shahada ya kwanza ya uuguzi wanaohitimu masomo ya kidato cha sita.
Kwa wale walio na elimu ya stashahada na uuguzi na ukunga, Shule hiyo inapokea wanafunzi wanaotaka kusoma wakiendelea na kazi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania (AKU) Dk Eunice Pallangyo katika maonyesho ya 18 ya vyuo vikuu nchini yaliyoratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yakiwa na kaulimbiu: "Kukuza ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, sayansi na teknolojia kwa uchumi imara na shindani.
“Tumejiandaa vya kutosha kutoa mchango wetu wa kutosha kwa wanafunzi watakaokuja kusoma kwetu. Programu zetu tuna imani kubwa kwamba sio wingi tu wa wanafunzi bali ni ule ubora wa wachache wanaoweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye jamii; hii ndio kitu tunatazama, tunapochukua wanafunzi wachache tunawapika na wanakuwa na mafanikio makubwa zaidi,
Mwanafunzi yeyote atakayekuja kusoma kwetu ategemee ubora na hatojuta, tuna vifaa vya ujifunzaji kwa vitendo kwa viwango vya juu na hata walimu wetu ni wale wa viwango vya juu kwa sababu tunawaandaa,”alisema.
Alisema chuo kimewekeza zaidi katika kuwajenga wataalamu, hivyo wataalamu wote watakaopikwa na chuo hicho watakuwa na weledi mkubwa na wenye ushindani kimataifa.
Dk Eunice alisema kuanzishwa kwa programu hiyo mpya ni kutokana na mahitaji ya wananchi, ambao wamekuwa wakiiomba chuo hicho kuanzisha shahada kwa wauguzi wanaotoka moja kwa moja kidato cha sita,
“Tuna uwezo wa kutosha wa kutoa mchango wetu katika eneo hili. Tumekuja na programu hii kutokana na maombi mengi ya watu, hivyo tunaamini mchango wetu sasa utaendelea kuwa mkubwa zaidi,”alisema.
Dk Eunice alisema wauguzi wengi na wakunga walikuwa wakiishia katika ngazi ya elimu ya stashahada, lakini sasa kupitia chuo hicho wanaweza kuendelea na masomo wakiwa kazini kupata ngazi ya juu ya elimu yaani shahada ambayo imeendelea kutolewa chuo hapo kwa muda mrefu sasa.
"Shule ya ukunga na uuguzi imeanzishwa nchini tangu mwaka 2000. Wakati wote tulikuwa tunafundisha masomo ya kuongeza ujuzi kwa wakunga na wauguzi walioko kazini na wale wa diploma.Tuna walimu na vifaa vya kisasa, kwa hiyo tukiwachukua wanafunzi hawa tuna uhakika watakuwa bora,’’ alieleza.