Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema-Bara), Tundu Lissu ameshindwa kuhudhuria kwenye mikutano mitatu ya chama hicho kutokana na matatizo ya kiafya.
Lissu ameshindwa kuhudhuria mikutano ya chama hicho inayoendea kufanyika leo Alhamisi Agosti 10, 2023 kuanzia asubuhi katika kata ya Nyanguge wilayani Magu, Mecco Manispaa ya Ilemela na katika kata ya Igoma wilayani Nyamagana.
Akizungumza katika mkutano wa pili wa hadhara uliofanyika Mecco Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema kiongozi huyo ameshindwa kuhudhuria kutokana na afya yake kuteteleka hivyo kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Bugando.
"Ndugu wananchi leo mlitarajia awepo makamu mwenyekiti wa chama lakini kutokana na matatizo ya kiafya ameshindwa kuungana nasi ila muda wowote anaweza kuungana nasi katika mikutano inayoendelea ila kwa sasa madaktari wamemwambia apumzike kwa saa tatu," amesema Msigwa
Mbali na kukosekana kwake wananchi na wafuasi wa chama hicho wamesema haijaathiri kitu kwani elimu iliyopatiwa na viongozi wa chama hicho imeeleweka na ujumbe uliokusudiwa umefika kwa wananchi.
Sawa Lissu hajaja lakini tumeelimishwa vya kutosha na viongozi wetu waliokuja na ujumbe umefika," amesema Mashaka Suleiman mkazi wa kata ya Igoma.