Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abood ammwagia pongeza Magufuli

DciEUf8XcAA55ch Abood ammwagia pongeza Magufuli

Wed, 4 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE mteule wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli kutokana na ushindi wa kimbunga wa asilimia 84.4 alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza na HabariLEO jana, Abood alisema ushindi huo unadhihirisha namna wanachama wa CCM na Watanzania kwa jumla wanavyoridhishwa na kazi kubwa aliyoifanya Rais Magufuli katika kipindi cha miaka mitano ya urais wake.

Alisema hatua ya Rais Magufuli kuwashughulikia mafisadi, watumishi hewa, kutoa elimu bure, kujenga mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la Nyerere Rufiji, kununua ndege, kujenga barabara nyingi za lami, kusimamia rasilimali madini zisitoroshwe nje ya nchi kumempandisha chati kwa kiwango kikubwa.

“Hii ndiyo siri ya ushindi huu wa kihistoria kwa sababu Watanzania wengi wameona namna alivyojitoa kwa ajili ya kuwatumikia kwa moyo wake wote, hivyo wameona hawana zawadi nyingine ya kumpa zaidi ya kumpa ushindi wa kimbunga na alistahili ushindi mkubwa kama huu,”alisema Abood ambaye ni miongoni mwa wabunge waliopata kura nyingi ambazo ni 171,339 akifuatiwa na Devotha Minja wa Chadema kura 14,139.

Alisema dalili za Rais Magufuli kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita zilianzia kuonekana tangu kwenye mkutano mkuu wa chama hicho baada ya wajumbe wote 1,822 wa mkutano huo kumpa kura ya ndiyo ili awe mgombea wa urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu.

Abood alisema ameguswa na utendaji kazi wa Rais Magufuli akisaidiana na wasaidizi wake Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwani wamefanya makubwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi waliyoinadi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

“Sisi wanaCCM na Watanzania wote tunatembea kifua mbele na tuna kila sababu ya kufanya hivyo kwa sababu viongozi wetu wakiongozwa na Rais Magufuli wamejitahidi kutekeleza yale waliyoahidi kwenye uchaguzi uliopita ukiangalia zahanati, vituo vya afya kila sehemu, elimu bure, ndege, mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere na barabara ndiyo usiseme,”alisema Abood.

Chanzo: habarileo.co.tz