Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT yaita uchaguzi kujaza nafasi ya Maalim Seif

Jn.jpeg NAIBU Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa ATC, Janeth Rite 

Wed, 27 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kinatarajiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa iliyoachwa wazi na hayati Maalim Seif aliyefariki dunia februari mwaka huu.

NAIBU Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Janeth Rite  amesema,  Halmashauri Kuu itakayoketi Oktoba 31 mwaka huu itatangaza mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo.

Alisema Halmashauri Kuu ya Chama Taifa ya ACT Wazalendo itaketi kwenye kikao chake cha kawaida katika ukumbi wa Hoteli ya Landmark  Dar es salaam na kitatanguliwa na Kikao cha Kamati Kuu itakayoketi tarehe Oktoba 30 mwaka huu katika Ukumbi huohuo.

"Hii ni Halmashauri Kuu ya kwanza kuketi baada ya Uchaguzi Mkuu 2020 ambao uligubikwa na udanganyifu, hila na hujuma kubwa.

"Hivyo basi, pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu ya Chama Taifa itapokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu 2020 na kuijadili" amesema Rithe.

Aidha Rithe aliongeza kuwa Halmashauri Kuu itapokea pia Taarifa ya Kamati Kuu ya Hali ya Chama katika kipindi cha  mwaka mmoja kwa maana ya tangu Oktoba 2020 hadi Oktoba 2021.

"Pia, kutokana na nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kuwa wazi kufuatia kufariki kwa Mwenyekiti wetu Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Halmashauri Kuu hii itatangaza mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa.

"Taarifa zaidi ya mchakato mzima wa uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo, itatolewa baada ya kikao cha Halmashauri Kuu.

"Halmashauri Kuu ya Chama Taifa itapokea pia Taarifa ya Hali ya Kisiasa ndani ya Chama, Nchi na Kimataifa, kuijadili na kutoa mwelekeo wetu wa kisiasa wa ndani na nje ya nchi" alisisitiza Mwenezi huyo.

Chanzo: ippmedia.com