Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT wataka mabadiliko sheria vyombo vya ulinzi

Duni Pic Data ACT wataka mabadiliko sheria vyombo vya ulinzi

Mon, 25 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kitafanya uchambuzi wa kina wa sheria na kanuni zinazoongoza Jeshi la Polisi, Vikosi vya SMZ na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuainisha mabadiliko ya kisheria yanayohitajika.

Hiyo ni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mageuzi ndani ya Jeshi la Polisi yanahitajika, yakiwamo ya kifikra ili jeshi hilo litoke kutoka chama hicho ilichokiita jeshi la kimabavu kwenda kwenye jeshi la kutoa huduma kwa raia.

Hayo yalisemwa jana na Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo wakati akihutubia kwenye kongamano la nne la kitaifa la tume huru ya uchaguzi kuelekea Katiba mpya mkoani Tanga

Duni alisema sheria zinazosimamia Jeshi la Polisi na vikosi vya ulinzi na usalama zinapaswa kurekebishwa kama walivyobainisha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya ACT Wazalendo ya mwaka 2020.

Alidai wanahitaji marekebisho ya sheria kandamizi ya Jeshi la Polisi Tanzania na huduma saidizi sura ya 322, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kifungu cha 43 (3), (4), na (6).

“Sheria hii pamoja na mambo mengine, inatoa mwanya wa wazi kwa polisi kuzuia uhuru wa kujumuika bila sababu yoyote ya msingi, hivyo kukengeuka Katiba yetu ya nchi ya 1977 ibara ya 20 (1) inayoruhusu uhuru wa kukusanyika,” alisema Duni

Advertisement Alisema mageuzi hayo yatakuwa sio ya kisheria tu bali kikatiba, kitaasisi na kifikra ili kuliondosha Jeshi la Polisi katika utamaduni wa kikoloni wa kutumia nguvu kubwa katika kutekeleza majukumu yake.

“Hivi sasa, Jeshi la Polisi limejijengea utamaduni sugu wa kutojali sheria kabisa. Licha ya sheria kuwataka polisi kuzingatia taratibu za kukamata, kupekua na kushika mali, kumekuwa hakuna mazingatio kabisa ya sheria,” alisema.

Aliongeza: “Ni jambo la kawaida kwa polisi kuvamia nyumba, kuvunja, kukamata, kupiga na kukamata mali bila hati ya kupekua (search warrant) na hati ya kukamata (arrest warrant),” alisema Duni.

Kauli ya Duni imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia Sululu Hassan amteue Jaji Mkuu mstaafu, Othuman Chande kuongoza kamati ya watu 12 itakayofanya kazi ya kuchambua na kutoa mapendekezo ya namna gani vyombo vya dola viwe ili viweze kuwatumikia wananchi.

Jaji Chande ataongoza timu hiyo ikiwa na sekretarieti ya watu watano.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa ACT Ado Shaibu alisema kama chama kimejenga heshima ya Tanga iliyokuwapo awali ilipokuwa ikitambulika kama eneo muhimu la viwanda na biashara.

“Tunataka mkonge na kilimo kwa ujumla wake viwanufaishe wakulima wake, tutaimarisha biashara na kuchangamsha Tanga,” alisema Shaibu.

Naye mjumbe wa Kamati Kuu, Ismail Jussa alisisitiza tume huru akisema, ndicho kinachopaswa kufanyika ili kuipata Katiba mpya.

Alisema endapo mchakato wa Katiba utaendelea ulipoishia kwa kuitisha kura ya maoni, watawahamasisha wananchi waikatae.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live