Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuifanya ukaguzi Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kama sheria zinavyotaka na taarifa yake iwe wazi kwa umma.
Wito huo umetolewa ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake ikijumuisha taasisi zilizo chini ya wizara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 20, 2023 na msemaji wa chama hicho katika sekta ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Muungano, Pavu Abdallah Juma, yapo malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma kwa baadhi ya watumishi.
Pavu amesema Takukuru inaingia kwenye kundi la taasisi zilizowekwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kiasi cha kushindwa kumulikwa ufanisi wake na mamlaka nyingine kwa kuwianisha na matumizi inayofanya.
“Takukuru inatengewa fedha na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha Takukuru, inapaswa kukaguliwa kila mwaka lakini tangu mwaka 2007 ilipoanzisha haijawahi kukaguliwa.
“ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuweka taarifa za fedha zinazojitegemea za Takukuru sio kufichwa kwenye fungu la 20 la bajeti. Pia, tunaitaka Serikali kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuifanya ukaguzi Takukuru kama sheria zinavyotaka na taarifa yake iwe wazi kwa umma,” inaeleza taarifa ya msemaji huyo.
Msemaji huyo amesema kutokana na uzoefu wa utendaji, historia na tafiti mbalimbali licha ya kuwa ni chombo kilichoanzishwa ili kuimarisha uwajibikaji na kuchunga matumizi mazuri ya rasilimali yapo malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi kwa baadhi ya watumishi.