Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT waitaka Serikali kukopa Sh 10 trilioni kumaliza kero ya maji

ACT.jpeg ACT waitaka Serikali kukopa Sh 10 trilioni kumaliza kero ya maji

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT Wazalendo kimependekeza Serikali ichukue mkopo wa Sh10 trilioni kwenye benki za maendeleo ili kusambaza maji nchi ili kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji Chama hicho kimetoa pendekezo hilo wakati kukiwa na mgawo wa maji katika mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine, jambo ambalo limekuwa kero kwa wananchi.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Oktoba 29, 2022 mkoani Dar es Salaam, msemaji wa sekta ya maji wa ACT Wazalendo, Esther Thomas amesema fedha hizo zikipatikana zielekezwe kwenye miradi ya maji nchi nzima ili wananchi wote wa mijini na vijijini wapate maji safi na salama.

Amesema mkopo huo wa muda mrefu utalipwa kwa makato ya tozo kwenye mafuta hadi utakapomalizika na lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata haki yao ya kupata maji safi.

"Serikali ichukue mkopo nafuu wa muda mrefu wa Sh10 trilioni kutoka Benki za Maendeleo ili kutekeleza mradi mara moja na mapato ya fuel levy (tozo ya mafuta) yatahudumia mkopo huo mpaka utakapomalizika kulipwa," amesema msemaji huyo.

Thomas amesema tatizo la maji nchini, siyo janga la asili ni uzembe wa Serikali katika kumaliza changamoto hizo. Amesema kuna miradi mingi ambayo ilianzishwa lakini hadi sasa haijakamilika.

Ameutaja mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe wenye uwezo wa kuzalisha maji lita million 103.7 na wenye kipande cha tatu cha kusambaza maji katika mji wa Mwanga kinachoghalimu Dola za Marekani 36.70 milioni, kipande kingine cha nne cha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji katika mji wa Same kinachotekelezwa kwa thamani ya dola 35.25 milioni.

"Mradi huu utekelezaji wake ulianza mwaka 2014, miaka nane iliyopita hadi sasa haujakamilika," amesema Thomas wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Mradi mwingine amesema ni wa uboreshaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika jiji la Mwanza na miji ya Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro 104.5 million.

"Licha ya kuanza kwa mradi baadhi ya maeneo bado watu wa Misungwi, Magu, Mkolani na Lamadi wanalia hawana maji safi yaliyo wafikia katika maeneo yao kama ilitarajiwa. Katika hili ni aibu kuona jiji la Mwanza ambalo asilimia 53.2 ya eneo lake limezungukwa na maji baridi, watu wake hawana maji," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live