Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT kugomea uchaguzi Serikali za mitaa usiposimamiwa na NEC

ACT.jpeg ACT kugomea uchaguzi Serikali za mitaa usiposimamiwa na NEC

Tue, 9 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kuwa hakitakuwa tayari tena kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, iwapo sheria haitabadilishwa kuidhinisha Tume Huru ya Uchaguzi (NEC), isimamie uchaguzi huo.

Hata hivyo, alipotafutwa, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amejibu kwa kukitaka chama hicho kutokuwa na hofu, kwani kila hatua itakwenda kwa wakati muafaka.

“Serikali imeshaweka bayana kwamba inataka kujenga nchi kwa kuheshimu maridhiano na ustahimilivu katika nyanja zote, ikiwemo ya demokrasia na siasa kwa ujumla. Hakuna sababu ya mtu yeyote au kikundi chochote kuwa na hofu,” amesema Matinyi.

Machi24, mwaka huu, chama hicho kilitoa tamko la kuitaka NEC ya sasa kujiuzulu kupisha kuundwa mpya itakayopatikana kwa utaratibu wa ushindani, hoja iliyojitokeza baada ya kulalamikia uchaguzi mdogo wa kata 22 uliofanyika kwamba haukuwa huru.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 5,2024 ,Waziri Mkuu Kivuli ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita amesema licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kusaini Sheria ya Uchaguzi, lakini wameshangaa katika hotuba ya Waziri Mkuu aliyoitoa Aprili 5 kutozungumzia ni lini watapeleka bungeni sheria ya kuidhinisha uchaguzi huo usimamiwe na NEC.

“ACT-Wazalendo hatutakuwa tayari tena kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaosimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baada ya uamuzi wa bunge kuondoa uchaguzi wa Serikali za mitaa kutoka Tamisemi na kuupeleke Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema Mchinjita.

Amesema kwa kuwa maandalizi ya uchaguzi ujao yanapaswa kufanyika sasa, msimamo wao ni kuitaka Serikali katika Bunge linaloendelea kupeleke Miswada wa Sheria ya Usimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa, ili uchaguzi huo usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi.

“Hatuelewi kwa nini hadi sasa Tume ya Uchaguzi iliyopo inaendelea kuishi na mchakato wa kuanza kuundwa tume mpya ya uchaguzi haujaanza, tunahoji hili kwa sababu sheria ya uchaguzi inatamka moja kati ya wajibu wa Tume ya Uchaguzi ni kusimamia uchaguzi wa Serikali ya mitaa,” amesema

Kuhusu jambo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wakili Anna Henga amesema chama hicho kina hoja ya msingi, kwani hata katika uchambuzi wao walioufanya walibaini sheria hiyo imekaa kiufundi zaidi, licha ya kusainiwa na Rais haiwezi kutumika bila kutungwa sheria nyingi ya kuleta tafsiri.

“Bila kutafsiriwa sheria hiyo haiwezi kutumika zaidi ya hapo uchaguzi huo utaendelea kusimamiwa na Tamisemi kulingana na sheria iliyopo, kama wameamua kugoma ni njia yao ya kuonyesha kwamba uchaguzi hautakuwa huru na haki,” amesema.

Henga ambaye ni mtaalamu wa Sheria amesema, “Kinachotakiwa tume iundwe ianze majukumu yake, lakini kwa sasa itakuwa ngumu kulingana na ilivyo kufika mwaka kesho, japo wakishinikiza inawezekana vitu vinaweza kwenda isipokuwa wakitaka kutumia sheria mchakato utachukua muda mrefu.”

Wakili Henga amesema ili jambo hilo liwezekane ni lazima muswada upelekwe bungeni na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi wateuliwe haraka, huku akisema ikipewa ifanye kazi NEC inayoishi sasa changamoto zitakuwa zilezile.

“Wajumbe wa hiyo tume hiyo inayoitwa tume ya mabadiliko au ya uajiri wa hiyo kamati ni watu ambao wapo na nafasi zao, ikiwemo majaji lakini wakienda kwa kusuasua hivi itakuwa mwakani hiyo,” amesema.

Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe amesema chaguzi zote zinatakiwa kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungo cha 10(1) c cha sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

“Ni lazima sheria ya serikali za mitaa ifanyiwe marekebisho, ili kuendana na sheria mpya za uchaguzi. Hata hivyo, binafsi niko kwenye maandalizi ya kwenda mahakamani kuomba Mahakama kuzuia uchaguzi wa Serikali za mitaa kufanyika hadi hapo sheria za serikali za mitaa zitakapofanyiwa marekebisho, ili uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Uchaguzi badala ya Tamisemi,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, Bubelwa Kaiza amesema chama hicho kiache uoga na kulalamika, huku akieleza kinachotakiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipeleke kanuni kuonesha namna itakavyoshiriki kusimamia uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live