Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo yataka marekebisho sheria ya habari

Vyombo Vya Habari Vinne ACT-Wazalendo yataka marekebisho sheria ya habari

Thu, 4 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kufuta sheria kandamizi, zinazonyima uhuru kwa vyombo vya habari na kutengeneza sheria mpya.

Taarifa ya Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi wa chama hicho, Philbert Macheyeki iliyotolewa leo Mei 3, 2023 ikiwa ni kuungana na wadau wa habari kuadhimisha miaka 30 ya uhuru wa vyombo vya habari imesema Serikali itengeneze sheria bora kwa kushirikiana na wadau.

Ambazo zitalenga kuleta uhuru, weledi, ukuaji wa sekta ya habari na kuachana na zinazopora uhuru wa vyombo hivyo.

“Tangu uhuru hadi sasa Tanzania imekuwa ikitunga sheria za habari zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na zinazokazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi,”amesema

Ametaja sheria hizo ni Sheria ya huduma ya habari 2016, Sheria ya Magazeti ya 1976, Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1977, Sheria ya kupata habari ya 2016, Sheria ya Mawasiliano ya kieletroniki na Posta ya 2010.

Sheria zingine alizotaja ni Kanuni za maudhui ya mtandaoni ya 2018, Sheria za makosa ya kimtandao ya 2015 (Kanuni za jumla za 2016), na Sheria ya Takwimu 2015 pamoja na marekebisho yaliyofanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya 2018.

“Utamaduni huu kwa muda mrefu ulizuia uhuru wa kutoa maoni, fikra na mawazo tofauti. Watu waliokuwa wanakosoa, walipitia wakati mgumu au kukosa jukwaa la kihabari la kueleza mawazo yao,”

“Hivyo vyombo mbalimbali vya habari; magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni (online media) hayawezi kuwa huru. Hali hii haijabadilika sana hadi leo tunapoadhimisha siku hii”amesema Macheyeki

Katika taarifa yake Macheyeki ameitaka Serikali kusimamia uanzishwaji wa baraza huru la habari nchini ili kulinda na kutetea haki na masilahi ya wanahabari.

“Kuanzishwa mchakato wa mabadiliko ya sera ya utangazaji na uandishi ili kulinda na kukuza uchumi na mazingira ya wanahabari wote,”

“Tunaitaka Serikali iratibu soko la mitandao ili kupunguza gharama za vifurushi vya intaneti kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya teknolojia ya habari nchini,”amesema

Chanzo: mwanachidigital