Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT Wazalendo yataka Wazanzibari kupigania nchi yao

ACTPIC 595x400 ACT Wazalendo yataka Wazanzibari kupigania nchi yao

Thu, 10 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Juma Haji Duni (Babu Duni), amesema umefika wakati kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu masula ya Muungano na kuwataka Wazanzibari kuweka tofauti zao kupigania maslahi ya nchi yao.

Duni alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wa hadhara Bumbwini wakati chama hicho kikihitimisha mikutano 12 ya hadhara iliyoanza tangu Mei mwaka huu kikizunguka kueleza dhamira ya chama hicho kutetea maslahi ya Wazanzibar.

“Tumechoka na ugomvi wa sisi kwa sisi, tunahitaji umoja tuunganishe nguvu zetu kama wewe ni CCM ubaki na UCCM wako kama mimi ni ACT nibaki ACT, lakini hayo yasituvuruge yanapokuja masula ya Kitaifa; tuungane tuwe kitu kimoja…lazima tutayarishe uzalendo wetu,” alisema Duni

Mwenyekiti huyo amesema “…wakati mwingine tunaonewa kwasababu tunataka wenyewe, kama hatuna umoja, na tunagawanyika kwa sababu ya maslahi ya watu wachache au vyama vyetu, hatuwezi tukafika tunapopata.”

Duni amesema umefika wakati wa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya Muungano, ili kila upande upate haki yake inayostahili na kwamba kusiwe na upande mmoja kuonekana unapata zaidi kuliko upande mwingine.

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Othman Masoud, amesema mwaka 2009 lilipitishwa azimio katika Baraza la wawakilishi kwamba suala la mafuta na gesi vitoke kwenye Muungano na baadaye 2016 wakapitisha sheria tena kukubali kwamba Zanzibar itachimba mafuta.

Hata hivyo amesema jambo hilo bado lipo kwenye Katiba ya Muungano ambapo ibara ya 64 inasema kama jambo limo ndani ya Katiba ni jambo la Muungano.

“Sasa leo unapotuambia kwamba kuna sheria au viongozi wamekubali mafuta yachimbwe, ikiwa na lengo la kutuaminisha Wazanzibari eti tuna mamlaka hiyo; ni kutukosea sana na wazanzibari, tunasema wakati wa kufanywa hivyo umepita na hautarudi tena,” amesema Othman.

Amesema iwapo jambo hilo bado lipo kwenye masuala ya Muungano kamwe haliwezi kufanikiwa kwa ukamilifu wake.

Hata hivyo Rais Hussein Mwinyi amekuwa akizungumzia suala hilo kwamba baada ya Zanzibar kukabidhiwa data ambazo zilikuwa zinahifadhiwa Tanzania bar, kwasasa Zanzibar imepata mamlaka kuendesha shughuli za utafutaji na uchimbaji mafuta yenyewe.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Ahmed Mazrui amesema Zanzibar haipaswi kuendelea kuwa nyuma, mna kwamba wanatakiwa kujiweka tayari kuhakikisha wanaiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Hata hivyo Mazrui amesema hilo halitafanikiwa iwapo hawataimarisha chama chao, “…lazima kila Mzanzibari ajue haki yake, tuhakikishe azma yetu ya kuifanya Zanzibar iwe Singapole ya Afrika, ibaki palepale kama alivyotaka marehemu Maalimu Seif Sharif Hamad.”

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho taifa, Ismail Jussa amesema licha ya kuhitimisha mikutano hiyo, lakini chama kinakwenda kujipanga upya kuendeleza moto wao kuibua udhaifu unaofanywa na viongozi, mpaka upatikane muafaka kuhakikisha wanaondoa utawala uliopo madarakani.

Chanzo: mwanachidigital