CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kimemkubali Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuwa anapenda amani, maridhiano, amechukua hatua kupambana na rushwa na amemsitiri vizuri aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Seif Sharif Hamad.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, alisema , chama hicho kitaendelea kufanya kazi na Rais Mwinyi kwa kuwa kinaamini pamoja na kwamba yapo mambo ya kiitikadi wanayofautiana, mfumo wa vyama vingi si vita, ila maridhiano.
Zitto aliyasema hayo jana asubuhi wakati akizungumza katika kipindi cha 360 cha kituo cha kituo cha televisheni cha Clouds.
Alisema kupitia Maalim Seif, walimfahamu zaidi Dk Mwinyi na dhamira yake kuwaunganisha Wazanzibari.
“Dk Mwinyi anapenda amani na maridhiano, amechukua hatua kukabili rushwa, amemsitiri Maalim Seif vizuri na kwa stahiki zote za kiserikali alizokuwa nazo. Watu wa visiwani wanapenda amani na si vita. Jambo kubwa kwao ni maridhiano na sisi kama chama ajenda muhimu kwa Zanzibar ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa na maridhiano,” alisema Zitto.
Alisema ili kudhihirisha dhamira ya kupenda maridhiano, Dk Mwinyi alipoanza kupanga safu ya uongozi, aliteua Baraza la Mawaziri katika wizara mbalimbali lakini aliacha wizara mbili (Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto) kwa ajili ya upinzani.
Zitto alisema Maalim Seif alisaidia kuwaongezea imani kuhusu Dk Mwinyi, kwani kupitia vikao vya chama na mazungumzo kati yake (Zitto) na Maalim Seif, walipokuwa na shaka kuhusu Dk Mwinyi, aliwaondoa hofu kuwa anamuamini.
Kingine alichokifanya Dk Mwinyi na kuwaongezea imani ni namna alivyopokea ushauri wa Maalim Seif, kutopelekwa katika Baraza la Wawakilishi Sheria ya NGO kwa kuwa ina mapungufu na kuagiza ifanyiwe kazi kwanza.
“Hii inaonesha huyu ni mtu anayesikiliza ushauri na alimwamini sana Maalim Seif kwamba wangefanya kazi kwa karibu na kuifikisha Zanzibar pazuri,” alisema Zitto.