Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT Wazalendo yapitisha wanawake 13 kuwania ubunge, uwakilishi

643c1970a7e69c4788890f5dca8fa6bc ACT Wazalendo yapitisha wanawake 13 kuwania ubunge, uwakilishi

Wed, 19 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMLA ya wagombea wanawake 13 wamepitishwa kugombea ubunge na uwakilishi kupitia Chama cha ACT-Wazalendo huku viongozi wakongwe wa kisiasa wakirudi tena katika nafasi zao kuwania majimbo ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa orodha ya wagombea wa chama cha ACT-Wazalendo iliyotolewa, wagombea 13 wanawake wamepitishwa kuwania nafasi hizo kwa upande wa Unguja, huku majimbo 18 ya kisiwa cha Pemba ambacho ni ngome yake kubwa, yamewasimamisha wagombea wanaume wote.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zahra Ali Hamad amepitishwa kuwania uwakilishi jimbo la Dimani. Anatarajiwa kuchuana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Zahra alisema ameamua kujitosa katika jimbo kwa ajili ya kupata changamoto za kupambana katika siasa na kuchaguliwa na wapigakura kama kipimo cha siasa.

“Nimegombea uwakilishi jimbo la Dimani na nashukuru nimepitishwa na chama changu kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba ambapo natarajia kupata upinzani kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi,'' alisema.

Mwanamrisho Taratibu Abama amepitishwa kuwania ubunge jimbo la Chumbuni huku Mtumwa Ali Makame atagombea ubunge jimbo la Tumbatu.

Katika jimbo la Malindi Unguja, Halima Ibrahim Muhamed amechaguliwa kugombea nafasi ya ubunge baada ya kuwaangusha vigogo, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ali Saleh na Ibrahim Sanya ambaye alishika nafasi ya kwanza katika kura za maoni.

Ismail Jussa amechaguliwa kukiwakilisha chama katika nafasi ya uwakilishi jimbo la Malindi. Waliokuwa wanasiasa wakongwe na wawakilishi wa chama cha CUF na baadaye kuhamia ACT-Wazalendo, Hamad Masoud na Hijja Hassan Hijja wamerudi tena katika siasa, baada ya CUF kususa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Pavu Abdalla Juma amechaguliwa kuwania uwakilishi jimbo la Donge ambalo ni ngome imara ya CCM.

“Nimepitishwa na chama changu kuwania nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Donge, nafahamu ni ngome imara ya Chama Cha Mapinduzi lakini nimejipanga kupambana na mgombea yeyote atakayeteuliwa na chama hicho,”alisema.

Mwandishi wa habari maarufu, Jabir Idrissa amepitishwa na Chama cha ACT-Wazalendo kuwania ubunge katika jimbo la Pangawe, huku mwanasiasa mkongwe, Juma Duni atawania uwakilishi jimbo la Chumbuni.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wiki ijayo itafungua pazia la kuchukua fomu kwa wagombea wa urais, uwakilishi na ubunge.

Chanzo: habarileo.co.tz