Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo yajitetea kwa Msajili

4a9968dbac0a193b09b634382bfe4d8a ACT-Wazalendo yajitetea kwa Msajili

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimekanusha kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kusisitiza kuwa Mgombea wake wa Urais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad hakumnadi wala kumuombea kura Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Kimebainisha hayo katika barua yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya kuandikiwa barua na Ofisi ya Msajili kikitakiwa kijieleze kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa, baada ya mgombea wake kumnadi Lissu katika mkutano wake wa kampeni.

“Tunapenda kueleza kuwa mgombea wetu wa urais Zanzibar, Maalim Seif hakiuka sheria na Kifungu cha 11 (a) kinachoweka utaratibu wa vyama kuungana na vinavyokusudia kuungana kabla au baada ya uchaguzi,” ilisema taarifa hiyo, iliyotolewa na Joran Bashange kwa niaba ya Katibu Mkuu wa chama hicho.

Ilisema Maalim Seif hakumuombea kura Lissu kama inavyodaiwa na ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Video clip uliyotutumia haina maneno hayo na nikuombe urejee kusikiliza upya kwa makini. Alichosema mgombea wetu ni imani yake kuwa Lissu atakuwa rais wa Tanzania, jambo ambalo liko wazi kutokana na mwelekeo wake wa kuungwa mkono na Watanzania walio wengi,” ilisema taarifa hiyo ya ACT-Wazalendo.

Ilidai uthibitisho kuwa Lissu anashinda urais,unaonekana na namna wananchi wengi walivyo na hamasa kubwa na kujitokeza katika mikutano yake ya kampeni inayoendelea. “Hilo si kosa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa,” ilidai taarifa hiyo.

ACT-Wazalendo imesema kitendo cha mgombea mmoja kuonesha imani yake kwa mgombea mwingine katika uchaguzi ni jambo la kupigiwa mfano kwa siasa za Tanzania licha ya kuwepo kwa ushindani wa kisiasa.

Wakati chama hicho kikiri kumkubali Lissu, nacho kimesimamisha mgombea wake urais, Bernard Membe ambaye hata hivyo baada ya uzinduzi wa kampeni alioufanya mkoani Lindi, hajaonekana jukwaani.

Kwa siku mbili sasa viongozi wa ACT –Wazalendo wameonekana kuvutana, kutokana na baadhi yao kumpigia chapuo Lissu, huku mgombea wao, Membe akijitanabaisha kuwa bado ni mgombea urais wa chama hicho.

Akiwa mkoani Tabora kwenye kampeni, Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto alisema wanatarajia kutoa msimamo wao juu ya ushirikiano wao wa kusimamisha mgombea mmoja wa urais Oktoba 3, mwaka huu.

Kutokana na kuwepo kwa vuguvugu la vyama hivyo kushirikiana kama alivyobainisha Zitto, juzi Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alivionya vyama vya siasa nchini vyenye nia ya kuanzisha ushirikiano wa kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu, kuwa vitakuwa vinajitafutia adhabu.

Chanzo: habarileo.co.tz