Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo yaipongeza mahakama ya Tanzania hukumu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi

57384 Actpic

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimeunga mkono uamuzi wa Mahakama  Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyobatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi vinavyowapa mamlaka wakurugenzi wa majiji, manispaa, halmashauri na wilaya kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC).

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo Ijumaa ya wiki iliyopita uliotokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa mwaka 2018 na mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe akidai wasimamizi hao ni kinyume cha Katiba na kwamba ni makada wa chama tawala (CCM).

Jana mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Aderladus Kilangi alitangaza kukata rufaa uamuzi wa mahakama kuu katika Mahakama ya Rufani .

Leo Jumanne Mei 14, 2019 katika mkutano wake na wanahabari Katibu wa Itikadi,  Mawasiliano, na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema uamuzi wa Mahakama Kuu ni wa kihistoria kutolewa katika suala la nzima la kuhusu mfumo wa uchaguzi.

Amesema uamuzi huo ni sahihi na unakwenda sambamba na matakwa ya Watanzania waliohitaji kwa muda mrefu kupitia tume mbalimbali zilizoundwa ikiwamo ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.

"Uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu shauri ya Wangwe unareflect (unaendana)na matakwa ya wananchi ambao wanahitaji mageuzi katika mfumo wa uchaguzi. Tunaipongeza Mahakama, Wangwe na wakili wake Fatma Karume kwa hatua hii," amesema Shaibu.

Pia Soma

Hata hivyo, Shaibu amesema hajashangazwa na uamuzi wa Serikali wa kukata rufaa kuhusu shauri hilo  na walitarajia ingefanya hivyo kama ilivyokuwa uamuzi wa Mahakama Kuu dhidi ndoa ya utotoni kesi iliyofunguliwa Rebbeca Gyumi.

" Rufaa ni haki yako hatukatai lakini wajue wanachokifanya ni sawa dhuluma kwa Watanzania kwa sababu shauri limebeba matakwa ya wananchi walio wengi," amesema Shaibu.

Chanzo: mwananchi.co.tz