Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT Wazalendo walalamikia mwenendo wa SUK

ACT.jpeg ACT Wazalendo walalamikia mwenendo wa SUK

Thu, 21 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakijaridhishwa na mwenendo wa uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), tangu kuanza kwa Serikali ya awamu ya nane.

Maelezo hayo yametolewa leo Desemba 21 na katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alipokuwa akitoa maazimio ya kikao cha kamati kuu iliyoketi juzi jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu, Zanzibar Charles Hilary amesema masuala yote yanayohusisha SUK yanashughulikiwa chini ya kamati ya pamoja ya umoja huo.

“Hii kamati haijatoa taarifa yoyote kuhusu SUK, sasa hayo maoni yao na wangepeleka katika kamati hiyo, ndio kazi ya hiyo kamati,” amesema Hilary.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 21 jijini hapa, Shaibu amesema: “Kamati kuu imesikitishwa na mwenendo usioridhisha wa SUK na kuelekeza hatua kadhaa madhubuti za kuchukua. Taarifa juu ya hatua hizo itawasilishwa wakati mwingine.”

Akijibu swali alilotakiwa kufafanua kuhusu uhusiano wa SUK, Shaibu amesema miongoni mwa makubaliano ya Rais Hussein Mwinyi na Maalim Seif Sharif Hamad enzi za uhai wake ilikuwa ni kushugulikia hoja tatu zilizotakiwa kuweka msingi wa kuimarisha SUK lakini hazikushughulikiwa.

Hoja hizo ni kuachiliwa huru kwa wafuasi waliokuwa wanashikiliwa kutokana na uchaguzi mkuu 2020, marekebisho ya mfumo wa uchaguzi pamoja na mfumo wa uendeshaji wa SUK. “Kwa hiyo tunapopima SUK tunatazama maeneo hayo.”

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza masuala yanayotia dosari uhusiano wa SUK ni pamoja na sakata la uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina na kikwazo cha kitambulisho za Mzanzibari Mkaazi katika uboreshaji wa daftari la kudumu la kupiga kura.

Tatu ni baadhi ya hoja ikiwamo kura ya mapema katika mageuzi ya Sheria namba 4 ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kutofanyiwa marekebisho kwa kuwa inatumika vibaya wakati wa upigaji kura.

Katika sheria hiyo kipengele cha 82 (1), kinaeleza ZEC itaweka utaratibu wa upigaji wa kura ya mapema na itafanyika siku moja kabla ya siku ya upigaji kura au siku nyingine kama itakavyoamuriwa na tume.

Kuhusu maazimio 10 yaliyotolewa na Kamati kuu ya chama hicho, Shaibu amesema yameweka msingi kwenye muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2023.

“Kwanza ni Tume huru ya uchaguzi kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule mkuu 2025, tume hiyo itumie watendaji wake wakati wa chaguzi badala ya wakurugenzi wa halmashauri. Pia viongozi wa tume hiyo wakuu wapatikane kwa usaili kabla ya kuteuliwa na mkuu wa nchi.

“Serikali inatakiwa kuboresha muundo wa tume hiyo kwa kuzingatia maoni ya wadau na kikosi kazi, utaratibu mpya wa ruzuku unaozingatia mapendekezo ya kikosi kazi,” amesema.

Maazimio mengine ni kupunguza madaraka ya msajili wa vyama vya siasa na kuongeza uhuru wa vyama, kuongeza uhuru wa kibajeti wa tume hiyo na masharti kwa vyama ya viwango maalumu vya ushiriki wa wanawake katika vikao vya kimaamuzi.

Pai, chama hicho kimeshauri mabadiliko madogo ya kikatiba kuanza sasa na kwamba Serikali iweke wazi ratiba ya mchakato huo.

Mbali na maazimio hayo, kamati hiyo ilikubaliana pia kufanya uchaguzi wa viongozi wa chama wa kitaifa katika mkutano mkuu Machi 2 hadi 3, 2024 na marekebisho madogo ya katiba ya chama hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live