Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT- Wazalendo waishangaa Serikali kukana ripoti yake ya elimu

20666 Pic+act+wazalendo TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kimesema kinashangazwa na wepesi wa Serikali kuikana ripoti inayoelezea kuporomoka kiwango cha wanafunzi wanaojua kusoma na kuandika licha ya ripoti hiyo kuandaliwa na wataalamu kutoka serikalini.

Jana, chama hicho kiliibua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kufichua Ripoti ya Utendaji ya Sekta ya Elimu (AESPR) ya mwaka 2017/18 ikisema kiwango cha kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la pili kimeshuka.

Muda mfupi baadaye, Wizara ya Elimu kupitia Kitengo cha Mawasiliano ilisema ripoti hiyo haikuwa na uhalisia na kwamba upimaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu uliofanywa mwaka 2017 na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) ulishirikisha sampuli kubwa na kuzingatia vigezo vya kitaifa vya upimaji na umeonyesha mafanikio makubwa.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu amewaambia waandishi wa habari leo Oktoba 3, 2018 kuwa kitendo cha Serikali kuikana ripoti hiyo inadhihirisha wazi wizara haikutaka umma uyajue masuala yaliyoibuliwa na ripoti hiyo.

“Hii ripoti ni ya wizara imeandaliwa na wenyewe iweje sasa waikanushe na kuikana?” Alihoji na kudai “Baada ya chama chetu kuweka wazi maudhui ya ripoti hiyo kwa malengo ya kuchochea mjadala wa kitaifa kuhusu ubora wa elimu yetu hasa katika kipindi cha miaka miwili ya kile kinachoitwa ‘elimu bure’ Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikakurupuka upesi na kuikataa na kuiita si ya kweli”.

Amesema jambo la msingi linalopaswa sasa ni kuangalia mazingira bora ya kuinua kiwango cha elimu kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu na kuangalia maarifa wanayopewa wanafunzi.

Amesema chama hicho kinaamini katika mambo makuu mawili, kwanza kuweka mazingira mazuri yatakayowawezesha wanafunzi kusoma na walimu kujituma na kisha kutupia macho kiwango cha elimu kinachotolewa na si vinginevyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz