Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo waingia na gia ya sensa

Aa2c3def731d9c702dee77917288f963 ACT-Wazalendo waingia na gia ya sensa

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kushiriki katika sensa ya watu na makazi.

Amesema lengo la sensa hiyo ni kuiwezesha serikali kupata idadi kamili ya watu wake kwa ajili ya kufikisha huduma za maendeleo.

Duni alisema hayo mbele ya timu ya uhamasishaji wa sensa pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu wa ACT Wazalendo wa Mkoa wa Kaskazini A, Unguja katika kijiji cha Shangani.

Alisema sensa ikifanikiwa vizuri ni hatua moja kubwa ambayo itafanikisha mikakati mingi ya serikali kuwafikia wananchi wake na kuwapatia huduma bora za kijamii na maendeleo.

Alifahamisha kwamba hakuna sababu ya sensa isifikie malengo yake ili idadi kamili ya wananchi ijulikane.

Mapema, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Salim Abdalla Bimani aliiomba timu ya sensa ya watu na makazi kuyashirikisha makundi yote ikiwemo vijana katika vyama vya siasa kwa lengo la kufanikisha kazi hiyo kikamilifu.

Alisema kwa muda mrefu sensa imeonekana kuwa na mwelekeo wa sura ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutowahusisha vijana wengine kutoka katika vyama vya upinzani ikiwemo kuwapatia ajira za muda za ukarani.

"Chama chetu ACT-Wazalendo tutahakikisha tunashiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi na tutajitahidi kuona makundi yote yanafikiwa na kuhesabiwa kwa ajili ya kuiwezesha serikali kupata idadi kamili ya watu wake kwa maendeleo ya taifa,'' alisema.

Mapema, Ofisa Uhusiano wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Safia Abdallah Ali alisema maandalizi ya sensa ya watu na makazi yanaendelea vizuri ambapo wamechukua hatua ya kuyafikia makundi mbalimbali na kufanya ushawishi katikia vyama vya siasa kuona wananchi wanashiriki vizuri.

Alisema sensa itafanyika nchi nzima na malengo ya serikali ni kuona hakuna mtu anayeachwa nyuma bila ya kuhesabiwa.

''Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali ndiyo iliyopewa jukumu la kukamilisha sensa na ndiyo maana tumekuja tukilenga kuyafikia makundi yote muhimu katika jamii ikiwemo vyama vya siasa kutokana na umuhimu wake,'' alisema.

Tanzania itafanya sensa ya watu na makazi Agosti 23, mwaka huu ikiwa ni mara ya sita kufanyika kuanzia mwaka 1967, 1978, 1988, 2002, 2012, na hivi sasa 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live