Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesema mchakato wa upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya unapaswa kuwa shirikishi, wazi na jumuishi.
Shaibu ametoa kauli hiyo kwenye Mikutano Mikuu ya Majimbo ya ACT Wazalendo katika majimbo ya Kaliua na Urambo Mkoani Tabora aliyokuwa mgeni rasmi mnamo Juni 22 na 23, 2023.
"Nimemsikia Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo hivi karibuni akisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya utasimamiwa na kuratibiwa na CCM. Hatutakubali hilo litokee. Hii si Katiba ya CCM, ni Katiba ya Watanzania, inapaswa kupatikana kwa mchakato wa wazi, jumuishi na shirikishi kwa makundi yote kwenye jamii," alisema Shaibu.
Shaibu ameongeza kuwa ni muhimu kujifunze kilichokwamisha mchakato wa Katiba Mpya mwaka 2014 ambapo alisema somo la kwanza ni kutanguliza mbele maslahi ya vyama dhidi ya maslahi ya Taifa. “Ni muhimu vyama vyote vya siasa na makundi yote muhimu kwenye jamii yashirikishwe katika kujenga muafaka wa kitaifa ili tusikwame tena," alisema Shaibu.