Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ACT-Wazalendo, CUF vyasusia uchaguzi Kwahani

CUF XACT ACT-Wazalendo, CUF vyasusia uchaguzi Kwahani

Fri, 17 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kususia uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kwahani mjini Unguja utakaofanyika Juni 8, 2024.

Sababu za kususia uchaguzi huo imetajwa ni mwendelezo wa chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kushinikiza watendaji waliopo kujiuzulu ili kupata makamishna wapya na sekretarieti mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo, wamekuwa wakishinikiza wajumbe wa tume wajiuzulu ili timu mpya ipatikane kutokana na mchakato wa sheria mpya unaotaka watu waombe, wafanyiwe usaili, majina yapelekwe kwa Rais ili kutangazwa kupatikana kwa makamishna wapya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jana Alhamisi Mei 16, 2024 imeeleza uamuzi wa chama hicho umefikiwa juzi, Mei 15, 2024 katika kikao cha kamati ya uongozi kilichoketi mjini Unguja kwa kuzingatia madaraka yake chini ya Ibara ya 72a (2) (a) ya katiba ya ACT-Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2024.

“Uamuzi huu umefikiwa kutokana na msimamo wa chama chetu baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, tunahitaji tume iliyopo ijiuzulu,” amesema Salim Bimani ambaye ni Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma.

Katika taarifa, Bimani amesema sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi inataka wajumbe wa tume wapatikane kwa njia ya Watanzania kuomba kufanyiwa usaili na Rais kupelekewa majina ya kuteua.

“Makamishna wa sasa wa tume hawana uhalali wa kuendelea kusimamia uchaguzi huu na zijazo,” amedai Bimani.

Wakati huohuo Chama cha Wananchi (CUF), kimeungana na ACT-Wazalendo kutoshiriki uchaguzi hadi mabadililiko ya tume yatakapofanyika.

“Hatushiriki Tume Huru haipatikani kwa jina, bali inatakiwa iwe kamilifu, moja kati ya vinavyotakiwa kufanyika ni yale makubaliano yatekelezwe ikiwemo Tume Huru kuajiri watumishi kwa mchakato maalumu.”

“Sasa bado suala hilo halijafanyika, kilichobadilika ni jina tu, kwa hiyo Tanzania hakuna Tume Huru ya Uchaguzi. Haya yakikamilisha tutakuwa na tume huru ya uchaguzi hatutakuwa na kikwazo chochote cha kutoshiriki uchaguzi,” amesema Mohamed Ngulangwa ambaye ni Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano CUF.

Katika hatua nyingine, vyama vya DP, NRA na Ada-Tadea vimesema vitashiriki uchaguzi na vimeshatoa maelekezo ya kuanza mchakato huo mjini Unguja.

“Ijumaa Mei 17 kamati kuu ndogo itaketi Unguja kujadili majina kisha Jumamosi kamati kuu itakayokutana Dar es Salaam itamthibitisha na kumteua mgombea,” amesema Hassan Kisbya ambaye ni Katibu Mkuu wa NRA.

Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema: “Nimeshatoa maelekezo Zanzibar kuanza maandalizi ya kumpata mgombea atakayesimama kuipeperusha bendera ya chama hiki,” amesema.

Mwenyekiti wa Ada-Tadea, Juma Ali Khatibu amesema wameshapata mgombea atakayesimama katika uchaguzi huo na Mei 17, atathibitishwa katika vikao vya chama hicho.

Uchaguzi wa Kwahani unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ahmed Yahya Abdulwakil kufariki dunia Aprili 18, 2024 kutokana na shinikizo la damu.

Chanzo: Mwananchi