Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

817 kuwania uongozi CCM Moshi Mjini

Ccm Moshiii 817 817 kuwania uongozi CCM Moshi Mjini

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, kimewaonya makada wanaopanga safu za uongozi katika uchaguzi wa ndani ya chama unaoendelea kuacha mara moja, na kuwataka wanachama wenye sifa na ambao wamejipima na kuona wanafaa kuwa viongozi, kujitokeza kuchukua fomu.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Juni 28, 2022, na Katibu wa CCM, Moshi Mjini, Ibrahim Mjanakheri wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusiana na uchaguzi wa viongozi ndani ya chama unaoendelea, ambapo Julai 2, 2022 utaanza uchukuaji fomu kwa ngazi ya wilaya.

Mjanakheri amesema katika uchaguzi hakuna nafasi ya mtu, bali zipo nafasi za chama cha mapinduzi na jumuiya zake, hivyo kuwataka wanachama wote wenye sifa, kujitokeza kuchukua fomu ya nafasi ambazo zimetangazwa.

"Kila mtu ambaye anaona katika nafasi zote ambazo tutazitangaza ana sifa ambazo zinatajwa kwenye katiba ya CCM na kanuni zake, anaruhusiwa kujitokeza kuchukua fomu, hakuna nafasi ya mtu kwamba yeye ndiye achukue fomu kuomba nafasi fulani, hapana, kila mwanachama anayo haki," amesema Mjanakheri.

Ameongeza kuwa, "Tunapoelekea uchukuaji wa fomu ngazi ya wilaya utakaoanza Julai 2 hadi 10 mwaka huu, nitoe wito kwa wanachama wote kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi ambazo tumezitangaza katika ngazi ya Wilaya."

Akizungumzia uchaguzi ngazi ya kata amesema Baada ya uchukuaji na urejeshaji fomu kufungwa Juni 20, jumla ya wanachama 817, walijitokeza kuchukua fomu kuomba kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama katika kata 21 zilizopo Moshi Mjini.

Amesema nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu mkoa ambaye anahitajika kila kata mtu mmoja, wamejitokeza wanachama 79, huku nafasi ya Mjumbe mkutano mkuu wa Wilaya waliochukua fomu na kurejesha wakiwa ni 235.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live