Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

2018 ulikuwa wa wanasiasa mitandaoni

34080 2018+pic Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabadiliko ya kidunia kupitia msukumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano ulionekana kuwa msaada katika kulinda uhai wa vyama vya upinzani hapa nchini.

Uzoefu unaonyesha kwa hapa nchini, mitandao yenye umaarufu na wafuasi wengi ni Facebook, Twitter, YouTube, WhatsApp na Instagram.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa gazeti hili, jukwaa hilo la siasa mitandaoni lilianza kuchukua nafasi baada ya Rais John Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa na badala yake kila mbunge afanye siasa jimboni kwake.

Lakini, hata mikutano ya ndani pia ilionekana kuzuiliwa, mojawapo ni tukio la kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu siku chache zilizopita.

Jaribio la kupingana na zuio hilo lilipingwa vikali, baadhi ya wanasiasa hususani upinzani wakikutana na mkono wa jeshi la Polisi.

Hata hivyo, wanasiasa hao walihamishia siasa zao katika jukwaa la mitanda ya kijamii. Kwa hapa nchini, mtandao wa Social bakers, unataja wanasiasa sita kati ya watu 20 wenye wafuasi wengi kuliko Watanzania wote wanaotumia Twitter.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete anaongoza akiwa na wafuasi 1,000,030 akifuatiwa na Zitto Kabwe(720,000), Halima Mdee(502,716), Januari Makamba(489,804), Rais John Magufuli(397,637) na Profesa Jay(341,871).

Wanasiasa wengine wenye wafuasi kutoka upinzani ni John Heche(Chadema), Ismail Jussa, Lazaro Nyalandu, Tundu Lissu(Chadema) anayeuguza maumivu ya risasi bado amekuwa akifanya siasa kupitia mitandao ya kijamii hususani Twiter na WhatsApp.

Matukio yaliyoibua mjadala kupitia hotuba za Rais John Magufuli, sakata la korosho, sakata la kikokotoo, hamahama ya wanasiasa kuingia CCM, ajali pamoja kampeni yalipewa uzito.

Mijadala walioanzisha mitandaoni ilipokelewa na kutengeneza mijadala kutokana na idadi kubwa ya watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii kwa sasa.

Februari mwaka huu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yanaonyesha Tanzania ilisema idadi ya watumiaji wa intaneti imefikia milioni 23 mwaka 2017, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya kile kilichorekodiwa miaka mitano iliyopita.

Pamoja na siasa kuhamia mitandaoni, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji aliliambia gazeti hili kuwa hali ya ujenzi wa chama inaendelea katika ngazi za vijiji.

Alisema makadirio ya wanachama waliopo hai hadi mwishoni mwa robo ya mwaka jana ilikuwa ni milioni nne lakini bado wanaendelea na ukusanyaji wa taarifa za wanachama wapya.

Dk Mashinji alisema hali siyo nzuri katika njia kadhaa za ujenzi wa chama. “Kwa ngazi ya chini, tunajivunia kufikia watanzania katika asilimia 68 ya vitongoji( misingi) vyote nchini. Lakini viongozi wetu katika maeneo hayo wanabandikiwa kesi na kukamatwa na Polisi,”alisema Dk Mashinji.



Chanzo: mwananchi.co.tz