Singida. Wagombea 12 wa vyama vya siasa nchini Tanzania wamejitokeza kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kuwania ubunge wa Singida Mashariki kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu.
Uchaguzi mdogo katika jimbo hilo utafanyika Julai 31, 2019 na tayari uchukuaji na urejeshaji fomu umeanza ukitarajiwa kuhitimishwa kesho Alhamisi Julai 18, 2019.
Kesho pia utafanyika uteuzi wa wagombea na Ijumaa Julai 19 hadi Julai 30, 2019 ni muda wa watakaopitishwa kufanya kampeni.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Justice Kijaji amelieleza Mwananchi jana kuwa waliochukua fomu na vyama vyao katika mabano ni;
Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK), Amina Ramadhan (DP) na Ayuni John (UDP).
Wengine ni Amina Mcheka (AAF), Maulid Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).
Pia Soma
- KESI YA KINA KITILYA: Serikali yapewa sharti kuongeza shahidi
- Bobi Wine atangaza kuwania urais Uganda mwaka 2021
- Usaili JKT waibua tishio homa ya ini mkoani Mtwara
- Fedha zilizopelekwa shule iliyoshika mkia kidato cha sita zadaiwa ‘kutafunwa’
Uchaguzi huo unafanyika baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kutangaza Lissu kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma na kutotoa taarifa ya mahali alipo.
Spika Ndugai aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea na mchakato wa kujaza nafasi hiyo.
Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu Septemba 7, 2017 akitibu majeraha ya risasi 16 alizomiminiwa akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea.