Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zitto avunjika bega, Magufuli ampa pole

2bb9c13e3bb8e054af0d092387f204d5 Zitto avunjika bega, Magufuli ampa pole

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli amempigia simu kumpa pole Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto aliyepata ajali ya gari juzi mkoani Kigoma.

Magufuli amemuombea heri Zitto apone haraka ;na pia amewashukuru madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya cha Kalya na Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, kwa tiba waliyompa mwanasiasa huyo.

Katika ukurasa wake wa twitter, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa aliandika, “Mheshimiwa Rais Dk John Magufuli amempigia simu na kumpa pole Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe aliyepata ajali ya gari jana mkoani Kigoma.

Amemuombea heri ili apone haraka na pia amewashukuru madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya cha Kalya na Hospitali ya Maweni kwa matibabu waliyompa”.

Saa kadhaa kabla ya Rais kumpigia simu, Zitto alieleza kuwa anaendelea vizuri na aliwashukuru wahudumu wa Kituo Cha afya Kalya.

“Ninaendelea vizuri. Ilikuwa ajali mbaya sana. Namshukuru Allah kwa kutuponya. Shukrani kwa wahudumu wa Kituo cha Afya Kalya licha ya changamoto. Huduma ya kwanza imetusaidia. Shukrani kwa madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Maweni Kigoma. Mimi na wenzangu mpaka sasa ni wazima”aliandika Zitto kwenye ukurasa wake kwenye mtandao wa twitter.

Kwa mujibu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto alipata ajali juzi mchana akiwa na wenzake wanne kwenye gari lenye namba za usajili T 360 DDV.

“Ajali hiyo imetokea Jimbo la Kigoma Kusini katika Wilaya ya Uvinza Kata ya Kalya alikuwa kwenye mwendelezo wa kampeni za uchaguzi” kiliandika chama hicho kwenye ukurasa wake wa twitter.

Taarifa kutoka Kigoma zilidai kuwa gari alilopanda Zitto, liligongana na gari lingine kwenye msafara wake na kupinduka papo hapo.

Ajali hiyo ilitokea Kitongoji cha Kabeba Kijiji cha Lufubu Tarafa ya Buhingu Wilaya ya Uvinza mkoani huo. Ilitokea wakati kiongozi huyo akiwa kwenye ziara za kampeni za mgombea ubunge na madiwani wa chama hicho.

Taarifa ya Ofisa Habari wa ACT Wazalendo, Arodia Peter ilieleza kuwa ajali hiyo ilitokea wakati Zitto akiwa njiani kutoka Kata ya Kalya kwenda Lukoma kwenye jimbo la Kigoma Kusini

Mkuu wa Wilaya Kigoma, Samson Anga alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 8.40 mchana.

Taarifa zaidi zilidai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni magari mawili waliyokuwa wamepanda viongozi wa ACT Wazalendo kugongana, kutokana na vumbi na kisha kupinduka.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Saimon Chacha alisema baada ya ajali hiyo, Zitto na viongozi wenzake walipata huduma ya kwanza kwenye Kituo Cha Afya Kalya.

Chacha alisema Zitto alipata majeraha katika bega la kushoto na alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni.

Wakati huo huo, Zitto na majeruhi wengine watatu, waliopata ajali hiyo juzi mkoani Kigoma,wamewasili jijini Dar es Salaam na kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, ambako ilibainika Zitto amevunjika mfupa wa bega la kushoto.

Akizungumza na HabariLEO jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Uenezi, Habari na Mahusiano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Janeth Rithe alisema kiongozi huyo na majeruhi hao, waliwasili jana jijini humo kwa usafiri wa anga na kupokelewa na gari la wagonjwa .

Alisema baada ya kufika hospitalini hapo, walifanyiwa vipimo na ilibainika kuwa Zitto ambaye ni Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, amevunjika mfupa wa bega la kushoto. Majeruhi wengine hadi jana jioni walikuwa wakifanyiwa vipimo ili kubaini tatizo.

“Kiongozi wetu alipata ajali (juzi),akiwa njiani kutoka kwenye kampeni Kata ya Lukoma kuelekea Kigoma Kusini, alipatiwa huduma ya kwanza katika Kituo cha Afya cha Kalya,Uvinza mkoani humo na kupewa rufaa ya kuja huku, gari la wagonjwa lilimpeleka moja kwa moja Hospitali ya Aga Khan na kupokelewa eneo la huduma ya dharura, alifanyiwa X-Ray bega la kushoto na likaonekana mfupa umevunjika, ila pia presha(BP) ilikuwa juu, anaendelea kutibiwa na hali yake inaimarika muda baada ya muda’’,alisema Rithe.

Majeruhi wengine wa ajali hiyo, wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo ni Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, Said Bakema, Katibu wa Jimbo la Kigoma Kusini, Soily Matete na Boaz Chuma, ambaye ni mwanachama wa chama hicho.

Chanzo: habarileo.co.tz