Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zijue hatari za homa ya mgunda, namna ya kuikabili

Nose Bleedoingg (600 X 392) Zijue hatari za homa ya mgunda, namna ya kuikabili

Sun, 24 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

‘Leptospirosis’ maarufu kama homa ya mgunda ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aina ya ‘Leptospira interrogans’ ambao huathiri wanyama na binadamu.

Kwa mujibu wa kituo cha kukinga na kudhibiti magonjwa (CDC), aliyeambukizwa bakteria hao asipotibiwa inaweza kusababisha uharibifu wa figo, meningitis (kuvimba kwa membrane karibu na ubongo na uti wa mgongo), ini kushindwa kufanya kazi, shida ya kupumua na hata kusababisha kifo.

Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu.

Mganga Mkuu mkoa wa Lindi, Heri Kyaga anasema ugonjwa huo unaoambukizwa kupitia mkojo na wanyama wa porini, uchunguzi umebaini walioathirika wamekuwa wakifanya shughuli zao shambani, huku wakichanganyika na wanyama, hasa kwenye matumizi ya maji.

“Ugonjwa ulipozuka ilikuwa tunaangalia vyanzo huku tukiendelea kutibu, Serikali ilituletea vifaa tiba na dawa kwa ajili ya kutibu wagonjwa tuliokuwa tukiwapokea na mpaka sasa hakuna maambukizi mapya tuliyoyapata,” alisema Dk Kyaga.

Mmoja wa waathirika wa ugonjwa huo ambaye kaka yake alifariki dunia, Aziz Mohamed alisema wamekuwa wakichangia chanzo kimoja cha maji kati ya wao na wanyama wanapokuwa mashambani sababu hakuna vyanzo vingine.

“Tulikuwa shambani, homa yake ikaanza ghafla kwa kutoka damu puani akaugua kama siku tatu hivi, baadaye tukaona tumpeleke hospitali na kufika huko alianzishiwa matibabu, lakini alizidiwa na akafariki dunia,” alisema Aziz.

Jinsi unavyoenea

Mtaalamu wa ufuatiliaji wa magonjwa (FELTP), Dk Ally Husein anasema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira, ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Anasema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo na wakati mwingine majimaji mengine ya mwili kutoka kwa wanyama wenye maambukizi au kwa kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi.

Anasema maambukizi yanaweza kutokea pia baada ya kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo, huku maambukizi ya ugonjwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

“Ugonjwa wa Leptospirosis huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira, ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi,” anasema.

Anasema bakteria hao pia wanaweza kuingia mwilini kupitia ngozi au utando wa mucous kupitia machoni, puani au mdomoni na kupitia ngozi yenye mikwaruzo.

“Mgonjwa aliyeambukizwa vimelea vya ugonjwa huu huanza kuonesha dalili katika kipindi cha kati ya siku tano hadi 14 na wakati mwingine dalili hutokea kati ya siku mbili hadi 30,” anasema.

Dk Husein anasema dalili za ugonjwa huo zinajumuisha homa, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, uchovu wa mwili, mwili kuwa na rangi ya manjano, macho kuvilia damu, kutoka damu puani pamoja na kukohoa damu.

Mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati anasema dalili za ugonjwa huo zinafanana na ule wa Marburg, lakini magonjwa hayo mawili yana vyanzo tofauti.

“Marburg inasababishwa na virusi ambavyo vinafanana na vile vya ebola, mara nyingi mgonjwa anakuwa anatokwa na damu nyingi na sehemu nyingi za mwili. Ukiupata ndani ya siku mbili mpaka 21 unaanza kupata dalili kama homa kali na damu kutoka kwenye matundu ya mwili,” anasema Dk Osati.

Anasema homa ya mgunda inatibiwa na dawa aina ya antibiotics, kama vile doxycycline au penicillin, ambazo mgonjwa hutakiwa kupewa katika hatua za awali.

“Hata hivyo homa hii inaweza kutibiwa kwa dawa hizo hizo hata kwa mgonjwa aliyezidiwa au walio na dalili kali zaidi, lakini ni muhimu awekwe chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya,” anasema.

Dk Osati alipendekeza watu kuacha kutumia maji yaliyotuama au hata yale yanayotembea kwa kuogolea au kuzama ndani ya maji ambayo yanaweza kuwa na mkojo wa wanyama au kutowagusa wanyama walioambukizwa.

Kwa mujibu wa CDC, ugonjwa wa homa ya mgunda hutokea kwa binadamu kwa kuanza ghafla na hupata homa na dalili nyingine na kwamba ugonjwa huo unaweza kutokea katika hatua mbili.

Wataalamu wanaeleza ugonjwa huo hutokea baada ya awamu ya kwanza pamoja na homa, baridi, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika au kuhara bado mgonjwa anaweza kupona kwa muda lakini akawa mgonjwa tena.

Awamu ya pili ikitokea, huwa ni kali zaidi, mtu anaweza kupata shida ya figo au ini au homa ya uti wa mgongo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema kutokana na ugonjwa huo Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine inaendelea kuchukua hatua, ikiwemo kutafuta watu wengine wenye dalili, ili kuwapatia huduma.

“Serikali inawaasa wananchi kutokuwa na hofu, kwani ugonjwa huu unaendelea kudhibitiwa,” anasema.

Waziri Ummy anasema pia wanatoa mwongozo wa kitaalamu wa jinsi ya kubaini wagonjwa zaidi na kuwahudumia pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili kujikinga.

“Kwa bahati nzuri ugonjwa huu unaweza kuzuilika na unatibika. Wizara inatoa wito kwa watu wote kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga, ikiwemo kuepuka kugusa maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa,” anasema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz