Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zifahamu sababu za vitambi na suluhisho lake

Kitambi Kabla ya kuanza kwa diet inashauriwa kufanya uchunguzi wa kitabibu

Tue, 31 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vitambi na uzito uliopitiliza ni moja ya changamoto inayowakabili watu wengi duniani.

Licha ya baadhi ya watu kuhusisha vitambi na utajiri, hali hiyo ina madhara mbalimbali kwa afya ya ikiwemo shinikizo la damu, ugumba na kisukari.

Dk George Munisi, mtaalamu wa masuala ya lishe kutoka Kigoma, anaeleza kuwa kitambi ni hali ya mwili kuwa na mkusanyiko mwingi wa mafuta usio wa kawaida.

“Mkusanyiko huu unaweza kutokea sehemu mbalimbali za mwili, mara nyingi sehemu ya tumbo na kifua, mkusanyiko huu ukizidi hutengeneza uzito uliopitiliza, hali inayoweza kudhooofisha afya,” anasema Dk Munisi.

Kwa mujibu wa tafiti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyo chapishwa juni 2021 kuhusu unene uliopitiliza, zaidi ya watu bilioni 1.9 wenye umri kuanzia miaka 18 wana uzito uliopitiliza na watu milioni 650 wana vitambi duniai kote.

WHO imeenda mbali zaidi na kuanisha kuwa wanawake ndiyo wanaongoza kwa kuwa na vitambi kuliko wanaume. Hii inasababishwa na asili ya miili ya wanawake kuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mafuta mwilini (excess fat).

Changamoto hiyo ya kiafya kutofautiana kutegemeana na ukanda wa maeneo watu wanaoishi. Mathalan, waishio mjini wana uwezekano mkubwa wa kupata vitambi kuliko watu wa vijijini.

“Wagonjwa wanaonifuata kupata matibabu ni wengi lakini inategemea na sehemu ninayofanyia kazi, nikiwa Moshi (Mkoa wa Kilimanjaro) napokea wagonjwa saba mpaka 15 kwa wiki, lakini nikiwa Kigoma napokea wagonjwa wachache,” amesema Dk Munisi.

Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha mtu apate shida ya kuwa na kitambi ikiwemo maumbile ya asili, jinsi, vichocheo vya homoni, vyakula na vinywaji pamoja na mfumo wa chakula,

Kila mwanandamu ana jinsi mwili wake umeumbwa kiasili, kuna wengine wana asili ya maumbile makubwa, kuna wengine wana maumbile madogo na wengine wana maumbile saizi ya kati.

Watu wenye maumbile ya makubwa huwa wanapata shida ya vitambi kwa wingi kwa sababu miili yao ina uwezo wa kuhifadhi mafuta (fat) kwa wingi na kuyaweka sehemu mbalimbali mwilini, hivyo kila chakula anachokula kinageuzwa kuwa mafuta.

Kundi la pili la watu wenye maumbile madogo, kwa mujibu wa Dk Munisi kwa kawaida hawa huwa wembamba na kiwango cha miili yao kubadilisha nishati kuwa mafuta huwa ni kidogo hivyo shida ya vitambi kwao huwa ndogo.

Miili ya watu wenye maumbile membamba haina uwezo unaotabirika wa kugeuza nishati kuwa mafuta hivyo wanaweza kuwa wanene na kurudi kuwa wembamba itategemea na nini wanakula.

Shida ya vitambi kwa watu hawa huwa ni ya wastani ukilinganisha na watu wenye asili ya miili mikubwa, anaeleza mtaalam huyo.

Jinsia nayo huchangia kitambi

Kwa mujibu wa WHO, wanawake wana uwezekano mkubwa wa kupata vitambi ukilinganisha na wanaume, hii ni kwa sababu wanawake kiasili wana uwezo mkubwa wa kutunza mafuta kwenye miili yao ukilinganisha na wanaume.

“Wanawake wana uwezo wa kutunza mafuta kwenye sehemu nyingi kama tumboni, mapajani, kwenye makalio, kifuani hadi kwenye mikono, wakati mwanaume mafuta mengi hujikusanya kwenye tumbo na maeneo ya kiunoni,” amesema Dk Munisi.

Baadhi ya homoni zinafanya kazi ya kubadilisha wanga kuwa mafuta, kama hivi vichocheo vikiwa vingi mwilini vinasababisha mafuta kuzalishwa kwa wingi, hivyo husababisha unene na mwisho kitambi.

Inaelezwa kuwa ulaji na unywaji usiofaa ni sababu nyingine inayosababisha vitambi ikiwemo vyakula vyenye mafuta mengi au wanga kwa wingi ambavyo huchangia mlundikano wa mafuta mwilini. Mshauri wa tiba asilia kutoka kampuni ya Healing at Home Consultancy (MSI), Matilda Kambangwa, anasema watu wengi wanaokuja kwake kutaka ushauri wa kupunguza vitambi huwa hawazingatiI kula mlo kamili.

“Unakuta mtu kwenye kila mlo lazima awe na chakula cha kukaanga au wanga kwa wingi, Halafu anategemea asipate kitambi,” anasema Kambangwa.

Matilda anasema kuna wimbi kubwa la watu wanaotaka kupunguza kitambi kwa kutumia dawa, lakini dawa pekee sio suluhisho kama mtu atashindwa kubadili mfumo wa maisha bali kuamua kula mlo kamili ili kupata mwili wenye muonekano bora.

“Kwenye suala la kupunguza vitambi hakuna njia ya mkato (short cut) ujue mwili wako vizuri kisha badilisha mfumo wa maisha anza kula kulingana na mahitaji ya afya yako,” anasisitiza mtaalam huyo.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa suluhisho la kudumu la vitambi linaanza na jitihada za mtu binafsi, maamuzi ya kudumu ya kuzingatia aina ya chakula unachokula kila siku.

Hata hivyo Dk Munisi anashauri kuwa kabla ya kuanza kufanya diet (kujinyima kula) ili kukupunguza kitambi ni vyema kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ili kujua chanzo cha kitambi. kama kinatokana na matatizo ya homoni, ulaji mbaya au asili ya maumbile ndipo ashauriwe njia za kufanya kukiondoa.

Kambangwa anashauri mtu mwenye kitambi apendelea kutumia mboga mboga na matunda, licha ya utofauti uliopo kwenye visababishi vya vitambi vyakula hivi vina faida nyingi kwa afya.

Kwa upande wa vinywaji, mtaalam huyo anashauri matumizi ya juisi za kupunguza mwili (slimming juice) kama vile juisi ya maji ya ndimu na asali, chai ya tangawizi, mdalasini, mchai chai na limao ambavyo hutumiwa asubuhi dakika 40 au saa 1 kabla ya kupata kifungua kinywa kingine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live