Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zambi aeleza sababu vifo wajawazito, watoto Lindi

C76249c48900b8f5b7975f6e783dec59 Zambi aeleza sababu vifo wajawazito, watoto Lindi

Thu, 27 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, amekanusha kuwa, vifo vya watoto wachanga na wajawazito mkoani humo vinasababishwa na kukosekana rasilimali fedha, idadi ndogo ya watumishi na ukosefu wa usafiri wa magari kubeba mgonjwa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha wataalamu wa afya kuhusu jinsi ya kupunguza au kuondoa vifo vya watoto wachanga na wajawazito mkoani humo.

Alisema matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na wataalamu wa afya kutofanyakazi kwa kushirikiana, hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma za afya.

“Wataalamu wa sekta ya afya hawana umoja, kila mtaalamu anafanya kivyakevyake, lazima vifo vitapatikana.

“Tatizo hapa hakuna umoja kati yenu ngazi ya mkoa na wilaya hali ambayo inasababisha huduma za afya kuzorota,” alisema.

Alisema miaka 1960 mpaka 1970, wataalamu wa afya walikuwa wachache, vituo vya afya vilikuwa vichache mkoani humo, lakini sasa serikali imeboresha huduma za afya kwa kuongeza vituo vya afya, watumishi na vifaa tiba.

“Vituo vya afya, zahanati vimejengwa kila wilaya mkoani hapa, wataalamu nao wanaongezeka kila kukicha. Tatizo linaloonekana hapa ni la kitaalamu hivyo mnaweza kuondoa na kuacha kutoa visingizio.”

''Serikali imeboresha sekta ya afya, lakini bado vifo vipo, tuendelee kujadili jinsi ya kuondoa tatizo la vifo hivyo, ila mzidishe umoja miongoni mwenu,'' alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Gwenchwelle Makange, alisema mwaka 2019 vifo vya wajawazito vilifikia 48 na watoto wachanga 640 mkoani humo.

Alisema wataalamu wa afya mkoani humo wameazimia kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito na kuzitaka halmashauri za wilaya zifanye matengenezo ya magari ya wagonjwa, ziandae mpango wa ujenzi wa majengo ya mama ngojea na kutenga vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za watoto wachanga (NCU).

“Mpaka kufikia Agosti, vifo vya watoto wachanga ni 156 na wajawazito 27, hali hiyo inaonesha kupungua ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema.

Dk Makange aliwataka wataalamu wa afya mkoani humo kununua vifaa tiba kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa ajili ya vituo vya afya ambavyo havina dawa.

Chanzo: habarileo.co.tz