Watu zaidi ya 185 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho pasipo malipo yoyote katika hospitali ya wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe baada ya shirika lisilo la kiserikali la Hellen Keller International kufadhili matibabu hayo.
Wakazi hao akiwemo Yusta Ndetewale,Luth Matandala na John Pondamali wamekiri kuanza kuona tena baada ya matibabu hayo hivyo wameishukuru serikali kwa kuwaletea fursa hiyo ya matibabu.
Frank Chiduo ni Mganga mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe amesema mpango huo umesaidia watu wengi kupatiwa huduma ya upasuaji wa macho hususani wazee ambao hupata changamoto ya macho kutokana na umri wao huku Dokta Saada Ludovick ambaye ni Daktari bingwa wa macho toka Wizara ya Afya akisema kuna takribani watu milioni 3 wenye tatizo la macho nchini kote hivyo wamelazimika kuanza kutoa huduma hiyo kupitia Hospitali za rufaa.
Naye meneja mradi wa Shirika la Hellen Keller International Athuman Tawakali amesema mradi huo ni wa mwaka mmoja na unatarajiwa kuwafikia takribani watu 900.
Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Claudia Kitta ametembelea kambi hiyo na kuwataka watu hao waliopatiwa matibabu kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili waweze kujitokeza kupata matibabu hayo.