Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zaidi ya dozi 680,000 za Chanjo ya COVID-19 zimetumika Tanzania

CHANJO ED (1) Zaidi ya dozi 680,000 za Chanjo ya COVID-19 zimetumika Tanzania

Thu, 7 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

SERIKALI imesema hadi kufikia Oktoba 5 mwaka huu, jumla ya watu 681,736 wamepatiwa chanjo ya UVIKO-19, sawa na asilimia 66 ya dozi zilizosambazwa nchini.

Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, ilibainisha kuwa serikali kupitia kamati zake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kuhakikisha elimu ya namna ya kujikinga na utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo inaendelea kutolewa kwa wananchi.

Waziri huyo amesema kuanza kwa kampeni ya jamii shirikishi na harakishi nchini kumesaidia kuongeza hamasa na mwitikio wa wananchi kupata chanjo, ambapo idadi ya wanaochanja sasa imepanda zaidi ya mara 10.

“Mafanikio haya ya kampeni yanatokana na kuongezeka kasi ya uelimishaji wa wadau katika sekta mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na idara yake ya Habari na Maelezo, wasanii wa sanaa zote, makundi mbalimbali ya kijamii yakiwamo ya vijana, wanawake, wazee, wanamichezo, vyombo vya dini na madhehebu mbalimbali na wanasiasa,” alisema.

Dk. Dorothy aliongeza kuwa suala la kuhamasisha wananchi kwa kwenda nyumba hadi nyumba limesaidia kuongeza kasi ya utoaji chanjo, huku vituo vya kutolea huduma hiyo vikiongezeka kutoka 550 hadi kufikia 6,784 vinavyotoa chanjo nchini.

Waziri huyo pia alibainisha kuwa Oktoba 4 mwaka huu, serikali ilipokea shehena ya chanjo za Sinopharm na kwamba inatarajia kupokea shehena ya pili kesho na kufanya jumla ya chanjo zote zilizopokewa kuwa 1,065,000.

Alisema baada ya taratibu za uhakiki kukamilika, usambazaji utaanza na zitawafikia wananchi katika vituo vyote ambavyo kwa sasa vinatoa huduma ya chanjo huku elimu ikiendelea kutolewa na upokeaji chanjo utaendelea kuwa wa hiari kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluh Hassan.

Waziri Dorothy alisema kwa sababu ya  uelimishaji na mwitikio mkubwa wa wananchi kupata chanjo, baadhi ya mikoa imemaliza mgawo wa chanjo za awali na imekuwa ikiomba mikoa ya jirani, huku akiwahakikishia wizara itatoa chanjo zote mapema ili kazi iendelee.

“Nitoe wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo katika maeneo yao kwani chanjo hizo ni salama, zina ufanisi na ubora unaotakiwa na matokeo ya uchanjaji tumeanza kuyaona kupitia hospitali zetu kwani wanaolazwa na vifo vitokanavyo na UVIKO-19 si tatizo kwa waliochanja ukilinganisha na wale ambao hawajapata chanjo," alisema.

Licha ya mafanikio hayo, waziri huyo alitoa wito kwa wananchi kuendeleza tabia ya unawaji mikono kwa maji safi, tiririka na sabuni mara kwa mara au utumiaji wa vipukusi, uvaaji barakoa katika maeneo hatarishi, kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu, lishe bora, kufanya mazoezi na kutumia fursa ya kupata chanjo ili kuondoa tatizo la ugonjwa huo.

“Niwapongeze sana viongozi wa mikoa na watoa huduma wote wanaoendelea kufanya kazi kwa nguvu zao zote na niwahakikishie kuwa serikali inawaona na inatambua mchango wao, naomba tusichoke, tusikate tamaa mpaka tutakapofikia lengo letu la kuwakinga angalau asilimia 60 ya wananchi wetu ili kuudhibiti kabisa ugonjwa huu, pia tuendelee kuwaepuka wapotoshaji na baadhi ya taarifa hususani kwenye mitandao ya kijamii," alihitimisha.

Chanzo: ippmedia.com