Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yaweka hadharani uchunguzi mtihani wa utabibu

Mitihani Pic Data Wizara yaweka hadharani uchunguzi mtihani wa utabibu

Tue, 7 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema Kamati iliyoundwa kuchunguza kuvuja mitihani ya utabibu imebaini kuwa mitihani ya mwaka wa pili ya programu ya utabibu ilivuja huku ikisema taratibu za kumfungulia mashtaka aliyehusika na uvujaji zinaendelea.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Desemba 6, 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichalwe imesema kuwa Kamati hiyo ilibaini kuwa mitihani ya programu zingine haikuvuja.

“Katika uchunguzi huo kamati imebaini kwamba mitihani ya mwaka wa pili (NTA level 5) ya programu ya Utabibu (Clinical Medicine) ilivuja. Mitihani ya programu zingine zote haikuvuja”.

Katika taarifa hiyo Kamati ilifanya uchunguzi kuanzia Septemba 06, 2021 hadi Novemba 30, 2021 na kukabidhi taarifa hiyo kwa Katibu Mkuu (Afya) huku ikieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinakamilisha taratibu za kumfungulia mashtaka aliyevujisha mitihani hiyo.

“Chanzo cha kuvuja kwa mitihani hiyo kimebainika na vyombo vya ulinzi na usalama vinakamilisha taratibu za kumfungulia mashtaka mkufunzi aliyethibitika kufungua mitihani, kuipiga picha na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii” imesema taarifa hiyo

Taarifa hiyo pia imesema kuwa chuo kilihohusika na kuvuja kwa mitihani hiyo kitachukuliwa hatua.

“Chuo kilichohusika na kuvuja kwa mitihani hiyo kitachukuliwa hatua kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili iwe fundisho kwa vyuo au taasisi zingine”

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa kamati imetoa mapendekezo kwa Wizara ya Afya na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) yatakayosaidia kuimarisha usalama wa mitihani.

Kupitia taarifa hiyo, imebainisha kuwa Wizara ya Afya inakamilisha maandalizi ya mitihani ya wanafunzi wa utabibu wa ngazi ya tano (mwaka wa pili) ambayo ilifutwa baada ya kuthibitika kuwa ilivuja.

“Mitihani hiyo itafanyika kuanzia tarehe 13 Disemba, 2021 pamoja na mitihani ya marudio kwa wanafunzi ambao hawakufanya vizuri katika mitihani ya awali. Ratiba za mitihani kwa kozi zote za afya zimetumwa vyuoni.” Imesema taarifa hiyo na kuongeza

“Wizara inawaelekeza wanafunzi kuwa watulivu na kuendelea kujiandaa na mitihani hiyo. Wizara inawaagiza wakuu wa vyuo pamoja na wasimamizi watakaoteuliwa kuhakikisha kuwa mitihani inafanyika kwa mujibu wa taratibu na miongozo iliyopo ili kuhakikisha usalama wa mitihani” imesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live