Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yawataka wauguzi, wakunga kujali utu

97f5a1d74a72e071a38c47accf4818d5 Wizara yawataka wauguzi, wakunga kujali utu

Sun, 21 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, amesema wauguzi na wakunga wanapaswa kuzingatia viapo vyao vya taaluma na kutoa huduma kwa kujali utu, heshima na upendo kwa wagonjwa wanaowahudumia.

Dk Gwajima alisema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga, Ziada Sellah, katika hafla ya kwanza ya kuwasajili wauguzi na wakunga wapya iliyofanyika katika Kituo Cha Maendeleo ya Uuguzi na Ukunga mjini Kibaha mkoani Pwani.

Alisema pamoja na mambo mengine, ubora wa huduma za uuguzi na ukunga hupimwa zaidi kwa uadilifu wa watoa huduma unaosaidia kuzingatia matumizi sahihi ya elimu aliyonayo mtaaluma kwa kuwa elimu bila maadili ni bure.

“Tukio hili litasaidia kutoa msisitizo kwa wanataaluma kutambua wajibu wao katika utoaji wa huduma huku wakizingatia maadili ya taaluma zao, kitendo hiki kilitakiwa kutekeleza kipindi kirefu kilichopita na ni vyema kikatekelezwa na taaluma zote za sekta ya afya nchini ili kuwafanya wahitimu kuheshimu taaluma zao,” alisisitiza.

Kuhusu kuboresha uwezo wa kutekeleza majukumu ya Baraza la Wauguzi na Wakunga nchini, Waziri Gwajima katika hotuba hiyo, alitaka baraza hilo kuzingatia ubora wa stadi na maadili ya taaluma ili kushuhudia mabadiliko ya ubora wa huduma za afya nchini.

“Tumeendelea kushuhudia changamoto nyingi za huduma zinazotolewa bila kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa wagonjwa; natoa msisitizo tena kwa wanataaluma wote wa sekta ya afya; zingatieni viapo vyenu,” alisema.

Aliwahimiza viongozi katika ngazi za mikoa na hospitali za rufaa waliopewa mamlaka na Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya Mwaka 2010, kuchukua hatua mapema panapobainika kuna upungufu katika utoaji wa huduma.

“Tekelezeni majukumu yenu haraka iwezekanavyo na kisha mtoe taarifa kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Makao Makuu kwa hatua zaidi, wadau wanapenda kushuhudia haki inapatikana mapema, kuchelewa kuchukua hatua panapotokea kunaleta picha na taswira mbaya kuwa, kuna kasumba ya kulindana, au kuna udhaifu katika usimamizi wa maamuzi,” alisema.

Gwajima alilipongeza baraza hilo kwa kuandaa tukio hilo na kuhimiza liwe endelevu kwa vile linatoa wasaa kwa wanataaluma kuelewa maana ya baraza na majukumu yake.

Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Abner Mathube, alisema sheria iliyounda baraza hilo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma salama za uuguzi na ukunga kwa kuwasajili wataalamu wenye sifa za kitaaluma na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, wanatoahuduma chini ya viwango vinavyotegemewa.

Wakati huohuo: Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Happy Masenga, alisema baraza linahakikisha leseni ya kutoa huduma za kitaaluma za uuguzi zinatolewa kwa waombaji waliopitia mafunzo yaliyokubalika kutoka vyuo vinavyotambulika na kufaulu mitihani ya usajili inayoendeshwa na baraza.

Masenga alisema tangu mwaka 2014, baraza hilo limekuwa likiendesha mitihani ya usajili na leseni ili kupima umahiri wa wahitimu kujiridhisha kama wana uwezo wa kutoa huduma salama kwa wateja na hadi sasa wahitimu 30,715 wamekwishafanya mitihani hiyo.

Katika hafla hiyo wauguzi na wakunga 839 waliohitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali na kufaulu mitihani ya usajili na leseni iliyofanyika Novemba, 2020.

Chanzo: habarileo.co.tz