Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yatoa ufafanuzi kusitisha tangazo la uzazi

18470 Pic+uzazi TanzaniaWeb

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetolea ufafanuzi barua yake iliyoliandikia Shirika la FHI 360 ikiliagiza kusitisha kutoa matangazo yanayohamasisha uzazi wa mpango.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya, imeviagiza vituo vya radio na runinga kusitisha mara moja urushwaji wa matangazo hayo hadi itakapoamuliwa vinginevyo.

Mtaalamu wa maradhi ya wanawake na uzazi salama wa Wizara ya Afya, Dk Ahmed Makuani alisema jana kuwa matangazo hayo ni ya wizara hiyo ambayo hutengenezwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Alisema kinachofanyika sasa ni kuyaboresha ili kutoa elimu, “Matangazo yote ni ya wizara ya afya, yanatengenezwa na wizara, lakini unapotaka kuyarusha hewani kuna gharama, hivyo Tanzania ina ushirika na watu wa Marekani. USAID inatoa fedha kupitia FHI ndiyo matangazo yanatengenezwa yakiwamo hayo ya tulonge afya,” alisema.

Alisema kinachofanyika sasa ni kuboresha matangazo hayo ili kutoa elimu na kuwa si lazima, bali ni hiari kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutenganisha nafasi kati ya mtoto mmoja na mwingine.

Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema kwa sasa Serikali inataka kuhakikisha ujumbe sahihi unafika kwa jamii.

Alisema kuondolewa kwa matangazo hayo kumesababishwa na Serikali kutaka kufanya marekebisho na kabla ya mwisho wa mwaka huu yatarudi.

Chanzo: mwananchi.co.tz