Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yatoa namba ya kupiga dharura za kiafya

Emergency Call Wizara yatoa namba ya kupiga dharura za kiafya

Tue, 26 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amezindua namba ya simu ya dharura itakayokuwa suluhisho la vifo vya wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga.

Namba hiyo ya bure 115 imezinduliwa leo Jumatatu, Machi 25, 2024 jijini Dodoma kwenye mkutano wa kimataifa wa Afya ya Msingi unawakutanisha wataalamu wa afya kutoka Afrika na ulimwenguni.

Mkutano huo wa siku tatu ni mara ya kwanza kwa mkusanyiko wa watalaamu wa afya kufanyika nchini Tanzania na pia ni mkutano wa kwanza wa kimataifa mkoani Dodoma.

Akizundua namba hiyo, Dk Biteko amesema itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama mtoto vilivyotokana na ukosefu wa msaada paleikiwamo usafiri wanapopata dharura.

“Ninawagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha namba hii inapatikana kwenye huduma zote za afya,” amesema Dk Biteko ambaye alimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan Kwenye mkutano huo.

Amesema mpango huo unaojulikana kama m-mama ulizinduliwa Aprili 6, 2023 na Rais Samia jijini Dodoma kwa lengo la kuwa na namba ya dharura katika sekta ya afya.

Dk Biteko amesema mpango ulianza kwa majaribio mkoani Shinyanga na sasa utaanza kwenye mikoa mingine mitano ukiwamo mmoja wa Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura kwa mama na mtoto.

Amesema mbali na jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya kwa ngazi zote za afya ya msingi na afya ya rufaa, alitoa agizo la kutaka viongozi kuwajali na kuwathamini walio chini yao.

Amesema tatizo la mfanyakazi mmoja lisiwe kigezo cha kuwavunja moyo wafanyakazi wote na ambao hawahusiki na kosa lililofanywa.

Pia, amezitaka wizara zinazohusika na afya kutunza miundombinu iliyojengwa na Serikali kuanzia majengo na vifaa na si kuviacha vichakae wakati fedha nyingi zimetumika.

“Tangu mfumo huu uliporasimishwa, zaidi ya dharura 60,000 zimesafirishwa na kwa sasa kwa rufaa zinazotolewa kituo kwa kituo tunapata dharura zaidi ya 5,500 kila mwezi ikiwa ni sawa na dharura 200 kila siku (masaa 24) na dharura 8 kila saa nchi nzima. Hii inaonesha uhitaji mkubwa sana wa usafiri wa dharura kwa wajawazito, walojifungua na watoto wachanga,” alisema.

Amesema m-mama inaratibiwa katika hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo. Kwa kupiga namba 115, waratibu wa m-mama katika kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.

“Napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo Touch Health na Pathfinder International kwa mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa wote,” amesema.

Amewataka washiriki wa mkutano huo kuweka mpango mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu iliyofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya afya ya msingi inatunzwa na miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.

Dk Biteko amewataka waainishe mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo, na njia nyingine za kudumisha afya bora.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Tanzania imepiga hatua kwenye sekta ya afya na suala la vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania ilikuwa na vifo vya mama na mtoto 556 kati ya 100,000, na WHO inataka vipungue hadi vifo 250. Lakini, jitihada zilizofanywa na watendaji kwenye sekta ya afya vifo vimepungua kutoka 556 hadi 104 na kuvuka lengo la WHO,” amesema.

Dk Mollel amewataka watendaji katika sekta ya afya kujiuliza maswali kama fedha na vifaa vinakwenda sawa kwenye maeneo yote kwa nini maeneo mengine hafanyi vizuri.

Amewataka kuangalia suala la matumizi ya fedha na uongozi kama viko sawa sawa.

Mkurugenzi wa m-mama Tanzania wa Vodafone Fondation, Dolorosa Duncan amesema wao kama sekta binafsi wanashirikiana na Serikali kuokoa vifo vya mama na mtoto.

Amesema Mei mwaka huu namba hiyo kwa mikoa yote ya Tanzania kwa huduma za dharura za mama na mtoto na ikifika Juni mwaka huu namba hiyo itatumika kwa dharura zote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live