Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yataja mambo 9 kukabili corona

2543abe33bebbcc749d2bca9e68e38ab Wizara yataja mambo 9 kukabili corona

Mon, 22 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetaja mambo tisa ya kuzingatia kukabili virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID- 19.

Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwenye wizara hiyo, Gerard Chami, jana ilieleza kuwa, licha ya wananchi kuchukua tahadhari, wazingatie kanuni za mtindo bora wa maisha ili kuondoa hatari za kiafya zinazodhoofisha kinga ya mwili.

Taarifa ya Chami iliwashukuru waumini na viongozi wa dini na madhehebu yote kwa kuliombea taifa kwa siku tatu dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID- 19.

“Rai yetu kwa Watanzania na wadau wote wa taifa hili ni kuendelea kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na kuchukua tahadhari zinazostahili katika kujikinga na magonjwa”ilieleza taarifa hiyo.

Chami alitaja mambo ya kuzingatia kukabili magonjwa ya milipuko ukiwemo COVID-19 kuwa ni pamoja na kupata lishe bora yakiwemo matunda na mbogamboga, kufanya mazoezi mara kwa mara na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya unapoona dalili za magonjwa.

Alitaja mambo mengine ya kuzingatia matumizi ya tiba asili zilizosajiliwa na baraza la tiba asili, kuwalinda walio katika hatari wakiwemo wazee, watu wanene, na wenye magonjwa ya muda mrefu, na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni.

Chami alitaja mambo mengine ya kuzingatia kuwa ni kuvaa barakoa unapopata au kutoa huduma kwa mwingine aliyeko umbali wa chini ya mita moja, na kutumia vipukusi (sanitizer) mara kwa mara hasa kama hakuna maji safi tiririka na sabuni.

“Pamoja na wizara kuweka nguvu zaidi katika kuendelea kutoa elimu ya afya kwa umma kupitia njia mbalimbali zikiwemo runinga, magazeti, mitandao ya jamii, n.k ni vyema kila mmoja akawa na utaratibu wa kupima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya”alieleza.

Chanzo: habarileo.co.tz