Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yaanika mikakati kukabili virusi vya corona

CORONA Wizara yaanika mikakati kukabili virusi vya corona

Fri, 1 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imesema imetoa mafunzo ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) kwa wataalamu wa afya 2,113 wa mikoa 11 nchini.

Vilevile, imesema imeimarisha uwezo wa kupima sampuli kwa watu wote wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huo, ikibainisha kuwa kwa sasa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imejengewa uwezo kwa kupatiwa mahitaji yote muhimu katika kupima virusi.

Akiwasilisha bungeni jijini hapa jana, makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema serikali imekamilisha ujenzi na uungaji wa vifaa katika jengo jipya kwa ajili ya kukabiliana na corona.

Alisema watumishi 120 wameajiriwa kwa muda ili kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na kwamba serikali imeandaa utaratibu maalum wa kuwaweka chini ya uangalizi wa siku 14 kwa gharama zao.

Waziri Ummy alisema upande wa huduma za matibabu kwa wagonjwa, serikali inaendelea kuwapatia matibabu wagonjwa wa corona na kwamba kwa Dar es Salaam, matibabu yanatolewa katika Kituo cha Magonjwa Hatari ya Kuambukiza Temeke, Kisoka-Mlonganzila na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Amana.

Alisema serikali pia inajenga kituo cha kisasa cha wagonjwa wa magonjwa hatari ya kuambukiza eneo la Kisoka-Mloganzila, Dar es Salaam.

“Makatibu tawala wa mikoa na wilaya zote Tanzania Bara wameelekezwa kuandaa maeneo maalum kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa katika mikoa endapo watajitokeza katika maeneo yao. Hadi Aprili 24 April, mwaka huu, jumla ya mikoa 17 ina vituo vya matibabu ya wagonjwa wa corona,” alibainisha.

Waziri huyo alisema mafunzo ya watumishi yametolewa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Rukwa, Songwe, Tabora, Dodoma, Tanga, Mbeya na Pwani na yanaendelea kwa mikoa iliyobaki.

Alisema wizara yake pia imeendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kujikinga na kutambua dalili za ugonjwa huu. Elimu hiyo imeendelea kutolewa kwa njia ya vyombo vya habari (magazeti, redio na runinga), mitandao ya kijamii, shuleni, vyuoni, nyumba za ibada na vyombo vya usafiri.

“Nawashauri wananchi kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali tunayowapatia ikiwamo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

"Tunaendelea kuwakumbusha Watanzania kuwa ugonjwa huu ni wa hatari na hauna kinga wala tiba, na njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huu ni kufuata maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na wataalamu wa afya kuhusu namna bora za kujikinga na ugonjwa huu,” alisema.

Waziri Ummy alisema katika kudhibiti na kuhakikisha kuwa ugonjwa huu hauathiri watu wengi zaidi, serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuweza kubaini wanaoonyesha dalili za ugonjwa.

“Hadi Aprili 24, 2020, jumla ya wasafiri 2,001,670 wamepimwa joto la mwili (thermol screening) ili kubaini kama wana homa ikiwa ni dalili za awali za ugonjwa huu na wasafiri 3,064 wamewekwa karantini katika maeneo mbalimbali hapa nchini kati yao 2,101 wamekamilisha muda wa siku 14 na kubainika kuwa hawana maambukizo na hivyo kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kawaida,” alifafanua.

Waziri huyo alisema katika kuhakikisha kuwa wasafiri wote wanaoingia nchini wanapimwa joto la mwili, serikali imenunua jumla ya vipimajoto 324 (vya mkono 307 na vya kupima watu wengi kwa mpigo 17) ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo ya mipakani ikiwamo viwanja vya ndege na bandari.

Corona iligundulika Desemba 31 mwaka 2019 katika Jimbo la Wuhan, China na hadi sasa watu 480 wameugua nchini, 16 wamefariki dunia na waliopona ni 197, na watu 283 wanaendelea na tiba kati yake 14 wako chini ya uangalizi.

Duniani watu zaidi ya milioni tatu wameambukizwa na kati yao, zaidi ya 200,000 wamefariki dunia katika nchi na maeneo ya utawala 185.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live