Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara ya Afya yapewa agizo na Waziri Mkuu kuhusu ajira za madaktari

Kassim Majaliwa?fit=749%2C537 Wizara ya Afya yapewa agizo na Waziri Mkuu kuhusu ajira za madaktari

Fri, 19 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto ifanye mapitio ya mwongozo wa uendeshaji wa vituo vya afya kuhusu upatikanaji wa watumishi ili madaktari bingwa wapatikane hadi ngazi ya wilaya.

Pia ameielekeza wizara hiyo ishirikiane na wadau kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa ajili ya watoto wachanga, pamoja na uwapo wa vyumba maalumu kwa ajili ya watoto wachanga wagonjwa, vifaa tiba na watoa huduma wenye ujuzi.

Alitoa maagizo hayo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi, mtoto, vijana na lishe Dar es Salaam jana. Waziri Mkuu alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, aliiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ihakikishe mitaala na shule zinawekeza katika kufundisha somo la uzazi kulingana na umri wa wanafunzi.

“Pia mamlaka za serikali za mitaa zisimamie mpango wa lishe kwa wanafunzi wa shule za kutwa. Lishe ni muhimu sana katika suala zima la kuimarisha afya ya uzazi,” alisema Majaliwa na kuongeza: “Wadau wote katika ngazi zote, wanatakiwa kuwekeza ipasavyo kwenye mifumo ya huduma za afya ya uzazi na mtoto ili tufikie malengo endelevu ifikapo 2030 ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1,000.”

Alisema Rais Samia amedhamiria kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto na kuzitoa bila malipo ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan inaonekana wazi katika kuimarisha huduma ya mama na mtoto.

Tunajenga vituo vya afya ambavyo vimewekewa miundombinu muhimu ya kutoa huduma ikiwamo jengo la mama na mtoto na chumba cha upasuaji,” alisema Majaliwa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima alisema uzazi wa mpango ni afua muhimu katika upunguzaji wa vifo vitokanavyo na uzazi na unasaidia kuboresha afya ya mama na kumfanya ashiriki vema katika ujenzi wa taifa na kuongeza kipato kwa familia.

Alisema kwa sasa matumizi ya uzazi wa mpango kwa takwimu za ndani unafikia asilimia 39 na lengo la kitaifa ni kufika asilimia 47 ifikapo mwaka 2023. Dk Gwajima alisema Tanzania ina vituo vya afya 911 na 491 kati ya hivyo vinatoa huduma za dharura za uzazi na mtoto timilifu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

Chanzo: Habarileo