Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara ya Afya yaomba Sh990 bilioni, fungu la MSD lapungua

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wizara ya Afya imeomba kuidhinishiwa Sh990.68 bilioni kwa ajili ya bajeti yake mwaka 2019/20 huku fungu la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) likipunguzwa kwa asilimia 16.

Kiwango kinachoombwa ni sawa na ongezeko la asilimia 9.7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2018/19 ambayo wizara hiyo iliomba Sh866.23 bilioni.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Mei 7, 2019 akiwasilisha bajeti hiyo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Sh546.89 bilioni zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo na Sh443.79 bilioni kwa matumizi ya kawaida.

“Katika kuimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la ebola lililopo Kongo, wizara imenunua na kusambaza vipimajoto 106 kwenye mipaka 31 iliyopo kwenye mikoa 14 yenye hatari ya kuingia ugonjwa huu,” amesema Ummy.

Akielezea utekelezaji wa majukumu ya wizara yake, amesema kwenye bajeti itakayokamilika mwezi ujao, itahakikisha chanjo zinazowatosha zaidi ya watoto milioni mbili wenye chini ya mwaka mmoja, zaidi ya wajawazito milioni 2.16 na wasichana 643,383 wenye kati ya miaka tisa na 14. Hadi Machi, amesema asilimia 98 ya watoto chini ya mwaka mmoja wamepewa chanjo husika.

“Wizara imeendelea kubuni mikakati na kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya  ngazi ya msingi,” amesema Ummy.

Wakati bajeti ya wizara hiyo ikiongezeka kwa asilimia 9.7 mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imebaini baadhi ya taasisi zimepunguziwa fedha ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2018/19.

“Baadhi ya taasisi hizo ni Bohari Kuu ya Dawa ambayo bajeti yake imeshuka kutoka Sh240 bilioni mwaka 2018/19 hadi Sh200 bilioni mwaka 2019/20 sawa na asilimia 16,”  amesema Petere Serukamba, mwenyekiti wa kamati hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz