SERIKALI imesema si wagonjwa wote wanaokufa kwa tatizo la kushindwa kupumua, vifo vyao vinasababishwa na virusi vya corona ( COVID-19).
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel jana .
Alisema tatizo la kushindwa kupumua linashika namba mbili nchini na duniani kwa ujumla na isilazimishwe kwamba kila anayeaga dunia kwa tatizo hilo chanzo ni virusi vya corona.
"Leo wagonjwa wote wanaokufa kwa kushindwa kupumua wanaonekana wamesababishwa na corona wakati tatizo hilo limekuwa likishika namba mbili kwa magonjwa yanayoongoza kwa vifo, kwa nini sasa ilazimishwe ni corona," alisema Dk Mollel.
Alisema mgonjwa mwenye kisukari au ugonjwa wa moyo dalili mojawapo ni kushindwa kupumua na kwa wagonjwa waliokuwa na tatizo la kuumua (niumonia) au pumu ambao pia wanashindwa kupumua kwa mwaka jana watu walisema wana corona, jambo lililosababisha kila aliyeshindwa kupumua kuonekana ana virusi hivyo wakati kuna niumonia inayosababishwa na bakteria na nyingine virusi.
Dk Mollel alisema kwa mujibu wa takwimu katika utafiti uliofanywa na Watanzania wakishirikiana na watu kutoka nje ya nchi katika mwaka 2006-2015, kujua visababishi vya vifo kilichokuwa kikiongoza kwa kusababisha vifo ni malaria asilimia 12.75, magonjwa ya kushindwa kupumua asilimia 10.08, HIV asilimia 8.4 matatizo ya damu asilimia 7.78 na matatizo ya moyo kwa asilimia 6.31.
Alisema Tanzania inapambana kudhibiti virusi hivyo vya corona na inaendelea kujilinda na kulinda watu wake huku ikitambua kuwa nchi jirani zimeathirika.
Dk Mollel alisema, mwaka huu hakuna taharuki kubwa kama mwaka jana, ambapo wakati huo virusi havikuingia Tanzania tu bali dunia nzima lakini kwa kutumia sayansi na Rais John Magufuli aliweza kutoa mwelekeo ulionusuru Watanzania .
"Huko nyuma walisema dunia nzima iwe lockdown lakini sisi tulisema tutafuata ushauri wa wataalamu wa afya lakini kutumia taratibu hizo kwa namna ambayo inaangalia hali zetu,"alisema.
Dk Mollell alisema masuala ya afya lazima kuangalia mila na desturi, hali ya uchumi wa nchi kabla ya kuwa na mkakati wowote kwamba wakati ni mwafaka au la kukubali kuangalia ugonjwa mmoja tu bila kuangalia suala la uchumi.
Alisema Tanzania iliangalia mbinu zote na ndiyo maana ikaja na mkakati wa aina yake ambao hata sasa dunia inafanya kama ambavyo Tanzania inafanya.