Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wivu wa mapenzi kupita kiasi ni chanzo cha matatizo ya akili nchini

Arguing 11 Wivu wa mapenzi kupita kiasi ni chanzo cha matatizo ya akili nchini

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: Mwananchi

Wakati takwimu zikionyesha kuwa tatizo la afya ya akili linazidi kuongezeka nchini, imebainika kuwa migogoro mingi kwenye ndoa na uhusiano inachangiwa wivu uliopitiliza wa wenza.

Matokeo yake ni kukithiri kwa talaka na hata matukio ya kufanyiana ukatili ikiwamo mauaji.

Oktoba 11 katika kitongoji cha Kanyabugulu mkoani Kagera, Emmanuel Mdende alimuua mkewe kwa kumkata panga nyumbani kwake akishuhudiwa na mtoto wake wa miaka 14, kwa kile alichodai mwanamke huyo alikuwa na mwanaume mwingine.

Julai 20, 2021 Jeshi la Polisi nchini lilitoa takwimu za mauaji nchi nzima kuanzia Mei hadi Juni mwaka huu, zikionyesha matukio ya mauaji yalikuwa 275 na kati ya hayo ya wivu wa mapenzi yalikuwa 21.

Ukubwa wa tatizo



Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu alisema idadi ya wagonjwa wa akili imekuwa ikiongezeka, mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2018 tulikuwa na wagonjwa 357,799 waliokwenda kupatiwa matibabu, 2019 walikuwa 380,000, mwaka 2020 walifika zaidi ya 500,000,” alisema.

Undani magonjwa ya akili

Dk Ubuguyu alisema kuna magonjwa zaidi ya 340 ya akili yaliyogawanywa katika makundi tofauti.

Wivu na afya akili

Mwanasaikolojia na mshauri wa uhusiano, Deogratius Sukambi anasema wastani wa kesi saba kati ya 10 zinazofika ofisini zinazohusu migogoro ya uhusiano na ndoa, zina uhusiano wa moja kwa moja na mmoja wao kuwa na dalili za tatizo la afya ya akili.

“Unapokuwa na migogoro ya uhusiano ambayo inachochewa na mmoja wao ama wote wawili kuwa na tatizo hili, huwa sio rahisi kutatua matatizo yao kwa kuwa hayana uhusiano na madai wanayoyatoa.

“Hapa ndio utaelewa ni kwa nini migogoro hii imekuwa ni shida sana kutatuliwa na marafiki, ndugu, wazazi ama viongozi wa dini nyakati hizi. Ni kwa kuwa wao huona ni migogoro tu ya kawaida na katika mchakato wa kuitatua wanajikuta wanaongeza tatizo,”alisema Sukambi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mental Health Tanzania na daktari wa magonjwa ya akili, Firmina Scarion alisema ukosefu wa maarifa kuhusu afya ya akili, unawafanya watu waingie kwenye matatizo na hata kuathiriwa na wenye matatizo hayo.

Anasema, “Tuna shida ya uelewa kuna magonjwa yanayogusa utu kama vile hasira, ukatili au unakuta mtu hawezi kukaa na mwenza kwa muda mrefu kwenye uhusiano, haya yote ni matatizo ya afya ya akili yanayohitaji kutibiwa.

“Sasa ikitokea mtu wa aina hii hajatibiwa si ajabu kusikia ndoa au uhusiano wake una changamoto za hapa na pale. Kwa hiyo ifahamike wazi kuwa hili ni tatizo na ukiona uko na mtu wa namna hii msaidie kupata matibabu au upate ushauri wa kuishi naye,” alisema Dk Scarion.

Kulingana na Sukambi wengi hupatwa tatizo la afya ya akili kuanzia miaka miwili hadi 18, katika kipindi hiki hupitia maumivu, kukatishwa tamaa na hali mbalimbali zinazomuachia majeraha moyoni.

Mchungaji wa kanisa la Neno la Unabii, Zakaria Masinga aliwataka wazazi kuwa sehemu ya mafunzo sahihi kwa watoto wao, ili kuwasaidia kusimama kwenye misingi imara na kuhakikisha wanapoingia kwenye ndoa, wanatawaliwa na upendo usiochuja.

“Maisha ya wazazi wa siku hizi yanachangia kuleta matatizo. Watoto wanashuhudia migogoro ya kila kukicha ya wazazi wao na hata kutengana vyumba, hivyo wanaona ndiyo maisha na kupeleka katika ndoa zao baadaye,’’ alisema.

Mauaji ya mapenzi

Hata hivyo, Sukambi anasema dhana ya wivu kuwa sababu ya mwenza kumuuwa mwenzake haina ukweli, bali wanaofikia hatua hio ni wale wenye tatizo la akili.

“Hakuna namna wivu unaweza kumfanya mtu amuue mwingine, ni mtazamo potofu uliopo kwenye jamii ndio maana hata tunasikia polisi wanasema fulani amemuua mpenzi wake kwa sababu ya wivu wa kimapenzi.

Hadi mtu anafikia kuua huo sio wivu lazima ana changamoto ya afya ya akili ndiyo inamsukuma kutekeleza dhamira aliyonayo,”alisema.

Unamjuaje mwenza mwenye tatizo la afya ya akili?

Wanasaikolojia wanasema ukimuona mtu ana wasiwasi dhidi ya mwenza wake, kutojiamini na anayehisi anasalitiwa, huyo ana tatizo la afya ya akili.

Gabriel Mselemu anasema aliwahi kuwa mwanamke nje ya ndoa, alikuwa na wivu unaokera.

“Huwezi kuamini mchepuko ulikuwa unapekua mpaka simu yangu. Kali kuliko zote siku moja ulinifumania na mke wangu kwa sababu hakuwa anamjua, lakini alikuwa ananifuatilia kiasi cha kuniudhi na kujuta kuwa naye”anasema Mselemu.

Anasema hata baada ya kumpa ishara kuwa yule ni mkewe, bado alichachamaa.

“Sitosahau hiyo siku na siamini kama ule ulikuwa wivu wa kawaida au kichaa, alikuwa hadi anataka kumpiga mke wangu amechachamaa, kila nikimwambia yule ni mke wangu hasikii anang’ang’ania yule mwanamke ameingilia uhusiano wetu, niliachana naye na kuanzia hapo sikutamani tena mchepuko,’ anasema.

Namna ya kuishi na mwenza mwenye wivu uliopitiliza

Sukambi anasema “Ukiwa unapenda kuishi na mwenza wako ambaye umeshagundua ana hili tatizo ni vyema ukakubali kufuata vitu vyote anavyotaka na kuacha vile unavyoona wewe vinafaa, ikishindikana ni heri kukaa mbali naye maana uwezekano wa kukudhuru ni mkubwa”.

Aliongeza; ‘’Bahati mbaya hata wenye tatizo hawafahamu kama wanalo, hivyo inakuwa vigumu kumsaidia matokeo yake ataona kama unamdharau, njia rahisi ni kufanya kila anachotaka au uamue kuwa naye mbali.

Kauli ya Sukambi inaungwa mkono na Matilda Manase anayesema kuwa alipata shida kwa miaka mitatu mfululizo kutokana na mabadiliko ya tabia ya mumewe.

Anasema mumwe alipata matatizo kazini na kusimamishwa kazi, “Shida ilianzia hapo, sikuwa napumua, alinifuatilia hadi ninapokwenda kukoga, nikirudi kazini ananifanyia upekuzi wa kunishirikisha na kuninyatia, achilia mbali kuninusa na kunusa nguo zangu, kibaya zaidi kila kitu nilichokuwa nacho alikihusisha na uhuni, usaliti.

“Nikirudi nyumbani anakuja kunidai na kukana kila kitu, kwa sababu hakuwa na tabia hizo awali, zilianza baada ya kusimamishwa kazi, wengi waliamini nimekuwa mkorofi kwa kuwa hana pesa kama zamani hivyo alikuwa akija tunasuluhishwa tunarudi huku nikionekana nina makosa karibu kila mara, mpaka alipoanza kunipiga sana ndiyo tukatengana”anasema Matilda.

Anasema haukuwa wivu wa kawaida, akianza kuzungumza macho anatoa macho na anakiamini anachokisema na wakati mwingine anahadithia kama filamu ya mizunguko yangu ya usaliti ambayo kiuhalisia haipo.

“Siku zote nilitamani familia yangu ielewe wakati ninaopitia, mara nyingi nilikuwa nikiamka ninamkuta macho ameshika kichwa, anasikitika au ananiangalia, hakika nilikuwa nahisi ataniua siku yoyote”anasema Matilda.

Chanzo: Mwananchi