Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma katika Hospital ya Rufaa Mwananyamala Dk. Saudan Masawe amesema wagonjwa wa magonjwa hayo wasinyanyapaliwe na jamii.
Kilele cha Siku ya Kifua Kikuu Duniani kinatarajiwa kuwa Machi 24 na Dk. Saudan amesema ugonjwa huo unatibika endapo mgonjwa huyo atawahi kupatiwa matibabu.
Dk.Saudan amesema jamii iwe na tabia ya kwenda katika vituo vya afya kupima wanapobaini kuwa na dalili za ugonjwa huo ili kupatiwa ushauri wa kitaalamu, kwani kufanya hivyo kutasaidia kujitambua na hivyo kuanza matibabu ya haraka ambayo hutolewa bure nchi nzima badala ya kuhusisha ugonjwa huo na Imani za kishirikina.
Daktari huyo akaongeza kuwa watu wengi wenye dalili za ugonjwa huo wamekuwa wakichelewa kufika katika vituo vya afya ili kupima afya zao kutokana na kuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina, hali inayosababisha afya zao kudhoofika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuamini kuwa wamelogwa hivyo kutumia muda mwingi kwenda kwa waganga.
Aidha Dk. Saudan akatoa wito unaowataka wananchi kutowanyanyapaa watu wenye kifua kikuu kwani ugonjwa huo unatibika kirahisi endapo mgonjwa atawahi kupatiwa matibabu kwa haraka na kwamba si kila mwenye kifua kikuu ana virusi vya ukimwi (VVU).
Siku ya kifua kikuu duniani mwaka huu imebeba kauli mbiu isemayo “KWA PAMOJA TUNAWEZA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU”