Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye ualbino waiomba Serikali iwatengee fedha za mafuta

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bariadi. Katibu wa Chama cha maalbino wilayani Bariadi, Juma John ameiomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwanunulia wenye ualbino mafuta ya kulainisha ngozi.

John ameyasema hayo leo Agosti 29 katika warsha ya kuwajengea uwezo na kujua haki za wenye ualbino wilayani humo.

Katibu huyo alisema, halmashuri ya wilaya ya Bariadi imekuwa ikiahidi mara kwa mara kutenga na kutoa asilimia 2 ya mapato kwa ajili ya kuwakopesha walemavu wakiwamo wenye ualbino, lakini haifanyi hivyo, wakati Serikali kuu ilishatoa mwongozo.

“Tunaendelea kuhimiza Serikali itoe fedha kwa ajili ya kutukopesha wenye ualbino tuwe na vyanzo vya mapato na tusiendelee kuwa ombaomba, tukiwa na miradi ya kujiingizia kipato tutajichanganya na jamii pia itaondoa unyanyapaa uliokuwa ukiendelea kulikabili kundi hili,’’ amesisitiza John.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Bariadi, Herbert Temba amesema kwa mwaka wa fedha 2017/18, halmashauri hiyo ilitenga na kutoa kiasi cha shilingi milioni tatu kwa ajili ya kununua mafuta ya kulainisha ngozi kwa watu wenye ualbino.

Ameongeza kuwa Serikali inalitambua kundi hilo na inafanya kila jitihada kuhakikisha wanawezeshwa ikiwemo kuendelea kutoa elimu namna ya kuanzishwa vikundi ili waweze kukopesheka.

Akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, ofisa utumishi halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Erick Sije, amesema watafikisha ombi lao katika mamlaka husika pindi Serikali itakapoagiza dawa, pia iagize na mafuta ya watu wenye ualbino ili waweze kuyanunua kwa bei nafuu.

Amesema lengo la Serikali ni kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu na kuwawezesha kupata mikopo ya riba nafuu ili waweze kuendesha maisha yao

Chanzo: mwananchi.co.tz