Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wengi waishi na kisukari bila kujijua

A40ae57f17a29854d72b209eb5cc059f Wengi waishi na kisukari bila kujijua

Sun, 15 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATU wengi wanaishi na ugonjwa wa kisukari bila kujijua, hatua ambayo madaktari na wataalamu wa afya wamehimiza wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao ili waweze kukabili ugonjwa huo.

Aidha, rekodi za Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA), zinaonesha zaidi ya watoto 4,000 wanaishi na kisukari huku kikitaja ugonjwa huo kuwa ni tatizo kubwa kutokana na idadi ya watu kuongezeka.

Meneja wa TDA, Happy Nchimbi alisema ili kupata takwimu hizo, chama kimekuwa kikiangalia vituo au kliniki ambazo zipo kwenye hospitali za mikoa zilizoanzishwa kwa jitihada za chama kusaidia watoto baada ya kugundulika kwamba wao pia wanapata kisukari.

"Mpaka sasa hivi chama hiki kimesharekodi takribani watoto zaidi ya 4,000 wanaishi na ugonjwa wa kisukari. Na katika hao, wapo ambao tayari wamepoteza maisha na wengine kwa njia moja au nyingine wamehama kutoka kwenye huduma za hospitali na wameenda kwenye tiba nyingine kwa sababu hawapatikaniki kwenye hospitali walizokuwa wanatibiwa hapo mwanzoni," alisema Nchimbi.

Akizungumzia hali ya kisukari, Nchimbi alisema takwimu za mwaka 2012 zilionesha kati ya watu 100, tisa wana kisukari. “Miaka nane imeshapita na tunavyofanya kambi ya kupima magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla bado tunagundua kuna watu wanaoishi na ugonjwa huo…Kibaya zaidi ni watu wengi kuishi na ugonjwa huo bila kujijua kwa sababu hauna dalili zile za moja kwa moja,” alisema na kuasa watu kupima afya.

Akielezea mwenendo wa ugonjwa huo, Mwenyekiti wa TDA, Profesa Andrew Swai alisema mwaka 1986/87 ulifanyika utafiti uliohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro na Mara, ulioonesha kati ya watu 100 wenye miaka 25 na kuendelea, asilimia moja ndio walikuwa na ugonjwa wa kisukari.

Profesa Swai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza Tanzania (TANCDA), alisema mwaka 2012 ulifanyika utafiti mwingine nchi nzima ukihusisha wilaya 33 na kubaini kwa kila watu 100 wenye miaka 25 na kuendelea, watu tisa walikuwa na ugonjwa wa kisukari.

"Kwa hiyo imepanda kutoka asilimia moja mpaka sasa asilimia tisa. Kuanzia mwaka 2012 haujafanyika tena utafiti kama ule, lakini tunawapima watu kama wanavyokuja kwenye makongamano kama haya tunawaambia waje kupimwa.

"Na tangu mwaka 2014 mpaka sasa tumeshapima watu zaidi ya 20,000, wote tunapima uzito, urefu, sukari na magonjwa mengine. Kwa hao takwimu zetu zinaonesha bado, ni kama asilimia tisa ndio watu wenye ugonjwa wa kisukari," alisema.

Profesa Swai alisema mwaka ujao wanategemea kufanya utafiti mwingine kwa nchi nzima, kwa kuwa wadau wao wameshakubali watatoa fedha.

Taarifa ya mwaka huu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kisukari iliyofanyika jana duniani kote, inaonesha katika kanda ya Afrika, zaidi ya nusu ya watu milioni 19 wanaishi na ugonjwa huu na hawajui kama wanao.

Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti katika ujumbe wake mwaka huu, anasisitia umuhimu wa kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa kisukari ili wafahamu visababishi, dalili na namna ya kuukabili.

Dk Moeti alisisitiza kuwa inawezekana kukabili kisukari kwa kuboresha mfumo wa maisha, ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi ya vinywaji vyenye sukari na kushughulisha mwili kwa takribani saa tatu kwa kila wiki kwa kutembea, kucheza muziki au kucheza mpira.

Mtendaji huyo wa WHO alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Wauguzi na kisukari’ kwa sababu wana nafasi kubwa ya kutoa huduma kwa watu wenye kisukari kwa kuwafanyia vipimo mara kwa mara na kuwapa msaada wa kisaikolojia. “Kwa pamoja tunaweza kukabili kisukari,” alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Kitaalamu, kisukari hutokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inayotakiwa. Miongoni mwa dalili za kisukari ni kuhisi kiu kila wakati; kwenda haja ndogo mara kwa mara; udhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati, kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.

Chanzo: habarileo.co.tz