Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri wa Afya akutana na Balozi wa Marekani nchini

Ummy 6.jpeg Picha ya Pamoja ya Ummy Mwalimu na Balozi Wright.

Wed, 2 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 02 Februari, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald Wright katika kikao kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya kwa kuainisha vipaumbele vyao katika eneo la afya kinga hususani eneo la mama na mtoto, lishe, masuala ya chanjo, kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kusisitiza uhamasishaji wa elimu ya afya kwa umma.

Waziri Ummy amebainisha kuwa kwa kutumia mfumo wa jamii shirikishi katika utoaji wa huduma ya chanjo ya UVIKO-19 maeneo ya huduma za umma utasaidia kuwafikia watanzania wengi kupata chanjo.

Kwa upande wake Balozi Wright amesema ushirikiano uliopo baina ya nchi yake na Serikali ya Tanzania ameahidi kutoa kiasi cha dola za kimarekani milioni 5 kwa Serikali ya Tanzania ili kufanikisha mpango mpya wa Global Vaccines wenye lengo la kuongeza upatikanaji wa chanjo nchini ili kuwalinda watanzania na maambukizi dhidi ya Uviko-19.

Mbali na hayo Balozi Wright ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa namna inavyokabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19 kupitia kuelimisha wananchi kuchukua hatua stahiki zinazoshauriwa na wataalam.

Aidha Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Marekani kwa ushirikiano wa muda mrefu na ameahidi kuimarisha zaidi ushirikiano kwa faida ya nchi zote mbili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live