Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri aanika mikakati viwanda kukabili corona

376 Bashungwa 660x400.png Waziri aanika mikakati viwanda kukabili corona

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WIZARA ya Viwanda na Biashara, imesema jumla ya viwanda na taasisi 12 nchini, vinatengeneza vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri Innocent Bashungwa alisema vifaa hivyo ni barakoa, vitakasa mikono na mavazi maalumu kwa watoa huduma za afya.

Alisema viwanda vidogo 55 vya nguo na mavazi pia vimeunga mkono kwa kuanza kutengeneza barakoa kwa kutumia malighafi ya kitambaa, na kwamba tayari kuna viwanda 40 vya kutengeneza vitakasa mikono vilivyosajiliwa hadi sasa.

Alisema katika kukabiliana na corona Machi mwaka huu, wizara yake ilikutana na wazalishaji wa malighafi ya kutengeneza vitakasa mikono (ethanol) na wazalishaji wa bidhaa hizo, lengo likiwa kujadiliana na wenye viwanda na wadau wengine namna ya kufanikisha utengenezaji na upatikanaji wa vifaa kinga vya kuzuia usambaaji wa ugonjwa huo.

“Viwanda hivyo vimeitikia wito wa kuunga mkono serikali katika vita dhidi ya ugonjwa huo. Kwa mfano, Kiwanda cha Kilombero kinachomilikiwa kwa ubia na serikali, kilichangia jumla ya lita 30,000 za ethanol kwa ajili ya kutengeneza vitakasa mikono na Wizara ya Afya ilipewa lita 20,000 na kiasi kilichobaki zilipewa taasisi za SIDO na TIRDO.

“Mwitikio huo umehamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza barakoa, vitakasa mikono, sabuni za kunawa mikono na ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa hizo," alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Trido ilitengeneza kitakasa mikono ambacho tayari kinatumika kwa jamii katika kujikinga na kuzuia kuenea kwa maambukizo ya corona.

“Mpaka sasa, Trido imetengeneza lita 202 za vitakasa mikono na kuwafikia watu mbalimbali kwa ajili ya matumizi.

“Wizara inaendelea na kazi ya ufanyaji tathmini ya mahitaji ya vitakasa mikono nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Mkemia Mkuu wa Serikali, wazalishaji wa ethanol na Mamlaka ya Chakula na Vifaa Tiba (TMDA)," alisema.

Waziri Bashungwa alisema kupatikana kwa takwimu halisi kutasaidia serikali kufanya uamuzi wa haraka hususan ya kuagiza ethanol ambayo ni malighafi muhimu katika kutengenezea vitakasa mikono.

AONYA WAFANYABIASHARA

Waziri huyo pia aliwaonya wafanyabiashara wanaotumia mazingira ya ugonjwa huo kama fursa ya kujinufaisha badala ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na janga hilo.

“Nawasihi wajielekeze katika kulinda afya za wananchi wetu kwani serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya aina hiyo,” alionya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live