Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amewatoa hofu wananchi kuhusu raia sita wa mataifa ya Denmark na Norway walioingia nchini humo jana Ijumaa Machi 13, 2020 wakitokea Kenya.
Kuwasili kwa raia hao kulizua sintofahamu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuhisiwa kuwa wana maambukizi ya ugonjwa wa mlipuko wa corona unaozidi kusambaa katika mataifa mbalimbali.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Jumamosi Machi 14, 2020 Waziri Ummy amesema raia hao walipokelewa jana Ijumaa saa 3 asubuhi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakitokea Kenya.
Waziri Ummy amesema kati ya wasafiri hao wanne walikuwa raia Denmark na wawili Norway. Kati yao wanaume walikuwa watano na mwanamke mmoja.
“Baada ya ukaguzi wa joto la mwili la wasafiri hawa unaofanywa na maofisa wetu wa afya kwenye kiwanja cha KIA. Mmoja wao aligundulika kuwa na homa ya nyuzi joto sentigredi 38 pamoja na kikohozi na mwili kuchoka.
“Katika mahojiano na wasafiri hawa, maofisa wa afya walibaini kuwa msafiri mmoja alikuwa na historia ya kukohoa lakini hakuwa na homa.”
Pia Soma
- Diwani aliyedumu katika nafasi yake kwa miaka 55 huyu hapa
- Kisutu imetengeneza jukwaa la siasa za mahakama kuelekea Oktoba 2020
- Kesi mpya wakurugenzi kusimamia uchaguzi yatua Mahakama ya Afrika
Amesema rai wote walichukuliwa sampuli zilizopelekwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyopo Dar es Salaam, kwa ajili ya uchunguzi ulionyesha watu hao hawana maambukizi ya virusi vya corona.
“Msafiri aliyekutwa na joto kali alibainika kuwa na mafua ya kawaida. Hadi sasa hali za wasafiri hawa wote ziko salama na wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao,” amesema Waziri Ummy
Waziri huyo ametumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa virusi vya corona (Covid-19) havijaingia Tanzania akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa na waache kusambaza taarifa zisizothibitishwa na Serikali