Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema abiria 16,800 waliotoka katika nchi zenye ugonjwa wa Ebola walichunguzwa na kufuatiliwa ambapo hakuna hata mmoja aliyeonyesha dalili za ugonjwa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema hayo jana Jumatatu Januari 20, 2020 wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya wizara yake katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 kwa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.
Alisema wizara iliendelea kuimarisha huduma za kinga katika maeneo ya mipakani kwa kuwajengea uwezo wataalamu, kupitia miongozo na kufanya uhamasishaji kwa wadau waliopo mipakani katika mikoa yote yenye mwingiliano na nchi ya DRC kwa lengo la kudhibiti kuingia kwa ugonjwa wa Ebola nchini.
Alisema jumla ya wataalamu 204 walijengewa uwezo wa utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambapo wadau 42 kutoka katika sekta ya usafiri na usalama walihamasishwa kuhusu udhibiti wa ugonjwa huo kupitia sekta ya usafiri.
Alisema katika kudhibiti magonjwa yanayotolewa taarifa kimataifa, jumla ya abiria wapatao 1,217,052 walichunguzwa katika mipaka yote nchini kuangalia kama wana magonjwa yoyote ya kuambukiza ikiwamo ugonjwa hatari wa ebola na homa ya manjano.
“Jumla ya abiria 16,800 waliotoka katika nchi zenye ugonjwa wa Ebola, walichunguzwa na kufuatiliwa ambapo hakuna hata mmoja aliyeonesha dalili za Ugonjwa,” alisema.
Pia Soma
- Nimr yazungumzia saratani kanda ya Ziwa
- Yametimia Samatta asaini miaka minne Aston Villa.
- Takukuru yarejesha Sh145 milioni za Amcos Mara
Amesema hatua za uthibiti ni pamoja na kutoa elimu ya afya kwa wananchi na upuliziaji wa dawa za kuuwa viluilui vya mbu.