Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Ummy ataka hospitali za mikoa, kanda kuongezewa uwezo

88441 Ummy+pic Waziri Ummy ataka hospitali za mikoa, kanda kuongezewa uwezo

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Tanzania,  Ummy Mwalimu ameitaka Taasisi ya Mifupa (Moi) kuzijengea uwezo hospitali za mikoa na kanda ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika taasisi hiyo.

Waziri huyo ameeleza kuwa taasisi hiyo inahudumia wagonjwa wengi ambao matibabu yangeweza kufanyika kwenye hospitali mikoa na kanda.

Akizungumza leo Ijumaa Desemba 13, 2019 wakati akizindua bodi ya wadhamini ya Moi, Ummy amesema ipo haja ya kuwekwa mikakati ya uhakika itakayowezesha kuziongezea uwezo hospitali hizo ziweze kutoa huduma za upasuaji wa mifupa wa kawaida.

“Tunataka Moi ipokee matatizo makubwa sio kama sasa ambavyo kwa mwezi inawafanyia upasuaji wagonjwa kati ya 700 hadi 900. Huu mzigo ungeweza kupungua endapo huduma nyingine zingekuwa zinatolewa katika hospitali za kanda na mikoa,” amesema Ummy.

Waziri huyu ameitaka bodi mpya kuhakikisha huduma zinazotolewa Moi zinaendelea kuboreshwa na mabadiliko yaonekane, kuipa jukumu la kuangalia namna wanavyoweza kupunguza gharama ya kumuona daktari na vipimo vya awali.

“Nimesikia kumuona daktari ni Sh50,000 naomba muangalie hii gharama ni kubwa. Sisi kazi yetu kutoa huduma, sio kutaka sifa ya kuwa tumeongeza mapato kumbe tunaleta kikwazo kwa watanzania maskini.”

“Tungependa kuona mabadiliko katika miaka mitatu inayokuja, bodi mpya ikasimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za Moi. Angalieni ni kwa namna gani mnaweza kujenga uwezo katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda,” amesema Ummy

Mwenyekiti wa bodi hiyo Profesa Charles Mkony amesema wajumbe wake wamejipanga kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kutoa huduma bora na kujiwekea rekodi katika nchi za Afrika Mashariki na kati.

Chanzo: mwananchi.co.tz