Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Ummy abeba ushauri, maoni ya wadau mjadala Jukwaa la Fikra

10314 Mwalimu+pic TZW

Fri, 29 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali itayafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wadau wa afya na washiriki wa mjadala wa maradhi yasiyoambukiza uliofanyika ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Mjadala huo wa Jukwaa la Fikra, ni wa kwanza kuandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Waziri Ummy amesema Serikali inapambana na maradhi hayo kwa kuhamasisha upimaji na kutoa elimu kwa wananchi.

“Tunatoa elimu kwa umma, tunahamasisha mazoezi. Tutaendelea kutoa elimu kuhusu ulaji usiofaa, pombe na matumizi ya tumbaku,” amesema.

Amesema Serikali itaweza kupambana na saratani ya kizazi baada ya miaka 10, kwa kuwa sasa kuna chanjo ya saratani hiyo.

“Chanjo hiyo ni salama, haihusiani na mtoto wa kike kukosa kuzaa, tutatumia vyombo vya habari kuhamasisha zaidi na kutoa elimu,” amesema.

Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kutoa huduma za kinga kwa kuweka wahudumu wa afya wawili katika kila kijiji ambao kazi yao itakuwa kuelimisha kuhusu kinga, chanjo na lishe.

“Tutaanza na wahudumu wa afya 600,” amesema.

Ummy amesema pia watajikita katika kinga, elimu kwa umma, huduma za uchunguzi na ugunduzi wa mapema.

Amesema kupambana na maradhi yasiyoambukiza kunahitaji rasilimali fedha, ndiyo maana nchi kama vile Afrika Kusini kodi inayotokana na vileo inaenda kwenye mfuko wa afya.

Waziri amewashauri waajiri kuwa na maeneo kwa ajili ya mazoezi katika ofisi ili waajiriwa kwafanye mazoezi.

Chanzo: mwananchi.co.tz