Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Ummy: Muswada bima ya afya upo hatua za mwisho

Ummy Muswada Waziri Ummy: Muswada bima ya afya upo hatua za mwisho

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha muswada wa bima ya afya kwa wote ambao unatarajiwa kupelekwa Bungeni wakati wowote kuanzia sasa.

Muswada huo ulioelezwa kwa mara ya kwanza ungepelekwa Bungeni Februari 2020 na Waziri Mwalimu wakati huo, umekuwa ukizungumzwa kufanyiwa marekebisho kwa vipindi kadhaa sasa hali iliyomlazimu aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kulivalia njuga akitaka ufafanuzi Bungeni Novemba 2021.

Ndugai alisema chenga za Serikali katika jambo la bima ya afya kwa wote zimekuwa nyingi na ziliwashinda wabunge kwa miaka mitano 2015/20 ambayo kati ya mikutano 19 na 20 walikuwa wakikumbushia lakini halikufanikiwa.

Kwa mujibu wa Ndugai ambaye Januari 2022 alijiuzulu nafasi ya Spika alisema, kama Bunge hili Serikali imeshindwa kupeleka muswada bungeni, ina maana mategemeo ya kupata ni Novemba 2022 ambao utakua ni mkutano wa tisa katika uhai wa Bunge la 12.   Hata hivyo, leo Alhamisi, Septemba Mosi, 2022 katika mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma uliolenga kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Waziri Ummy ametoa mwelekeo mwingine.

“Tupo katika hatua za mwisho sana kuleta huu muswada na nitawaomba wananchi wawe tayari kujiunga na bima ya afya kwa kuwa ugonjwa hausemi leo au kesho utaumwa unakuja bila taarifa.

“Tutakuja na kiwango kidogo cha kuchangia ambacho siwezi kusema sasa hivi, tutaweka kiwango tumefanya tathmini ya mfuko ifike mpaka miaka 10 au 30, tuingize watu wangapi, kwa mwaka watu wachangie kiasi gani na tutakuja na kiwango kidogo ambacho Watanzania wataweza kukimudu na hicho kiwango kitakuwa kinaonyesha wazi ni kiasi gani kinahitajika,” amesema Waziri Ummy.

Amesema licha ya bima ya afya kuwa lazima hakuna mwananchi ambaye atatozwa faini, kukamatwa au kuwekwa ndani bali itafungamanishwa na baadhi ya huduma za muhimu kama kitambulisho cha nida, pasipoti, leseni na huduma nyinginezo.

“Kila mwananchi atapata huduma mpaka ngazi ya taifa kama anavyopata mtumishi wa Serikali hili tupo mwisho kabisa kuhakikisha tunatengeneza sheria,” amesema Waziri Ummy.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ulioangalia uwezo na utayari wa wananchi kulipia bima ya afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa afya kwa wote, umeonyesha asilimia 73 wapo tayari kujiunga na mifuko ya bima ya afya.

Chanzo: Mwananchi