Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Ummy: Idadi ya wanaochanja chanjo ya UVIKO-19 imeongezeka

Waziri Ummy Mwa Waziri Ummy: Idadi ya wanaochanja chanjo ya UVIKO-19 imeongezeka

Fri, 8 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imeelezwa kwamba baada ya kutumia mbinu mbalimbali za uhamasishaji na elimu jamii juu ya chanjo ya UVIKO-19, idadi ya waliochanjwa nchini, imeongezeka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 13 katika kipindi cha wiki tano.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ameyasema hayo kwenye kikao kazi cha mapambano na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kushiriki chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Waziri Ummy amezitaja mbinu hizo za uhamasishaji na uelimishaji ni pamoja na matangazo katika magazeti, runinga, radio, vipeperushi, matukio makubwa na kuwa mbinu hizo zimeonyesha matunda.

“Kabla Ted (Dkt Ted Chaiban-Mratibu Mkuu wa kimataifa wa Chanjo Duniani) hajafika nchini, tulipokutana naye Geniva Mei tulikuwa tumechanja asilimia 6.8 baada ya kutumia mbinu hizi kwenda kwa jamii na matamasha tumefikia asilimia 13,” anasema.

Hata hivyo, anasema kama kuna mzazi ama mlezi mwenye mtoto wake mwenye umri wa miaka 12 hadi 17 ambaye anataka apate chanjo ya Uviko-19 basi ampeleke akapate chanjo hiyo.

Pia, Waziri Ummy anasema wamemweleza Dkt Chaiban na ujumbe wake kuwa asilimia 50 ya watu wanaoishi Tanzania wana umri mdogo chini ya umri wa miaka 18, hivyo asilimia 70 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ni milioni 21.4. Anasema hadi kufikiwa watu milioni 8.5 ambao ni sawa na asilimia 27 walikuwa wamechanjwa chanjo ya Uviko-19 na hivyo bado kuna kazi ya kufanyika ili kufikia lengo.

Ummy anasema hadi Juni 5 mwaka huu Tanzania kulikuwa na visa saba vya Uviko-19 lakini hadi kufikia Juni 6 kulikuwa na visa 14 na kuwataka watu kujitokeza kwa wingi kuchanja.

Naye, Mratibu Mkuu wa kimataifa wa chanjo Duniani, Dkt Ted Chaiban amewataka Watanzania wenye umri wa zaidi ya miaka 18 kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo hiyo kwasababu kwa kufanya hivyo kutawezesha mtu kujikinga wenyewe na familia yake.

Dkt Chaiban anaeleza kwamba UVIKO-19 ni ugonjwa ambao umeua watu milioni 6.3 ulimwenguni na kumekuwa na visa zaidi ya milioni tano vya ugonjwa huo duniani na visa hivi vingi vimefanya watu wengi kuwa mahututi na kulazwa hospitalini.

“Njia pekee ya kufungua Tanzania kiuchumi bila kuvaa barakoa na hatua nyingine za kujikinga ni kujitokeza kwa wingi kuchanja,” anafafanua Dkt Chaiban.

Anayataja makundi ya wafanyakazi wa sekta ya afya, watu wenye magonjwa sugu na wenye umri zaidi ya miaka 60 kuwa wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo.

Dk Chaiban anasema kuwa mapambano hayo yanawezekana ikiwa kila mmoja ataelekea katika mwelekeo mmoja wa kuhakikisha anashiriki kwenye mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Hata hivyo, amevitaka vyombo vya habari nchini kuwaelimisha Watanzania kutegemea sayansi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwani Tanzania inatumia njia za kisayansi kwenye mapambano hayo.

Kwa upande wake, mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, (RMO) Dkt Damas Kayera anaeleza kuwa hadi sasa watu 135,000 wameshapatiwa chanjo ya UVIKO-10 kwenye mkoa huo. Dkt Kayera anasema kuwa watu hao 135,000 ni sawa na asilimia 30 ya watu 669,516 wanaotarajiwa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 Mkoani Manyara.

Mkazi wa mjini Babati Mkoani Manyara, Hamis Seif amempongeza Waziri Ummy kwa namna alivyosimama kidete na kupambana tangu mwaka 2020 janga la UVIKO-19 lilivyoingia kwa mara ya kwanza hapa nchini.

“Kwa taaluma Waziri Ummy ni mwanasheria ila kwa namna anavyopambana na kuhakikisha Wizara ya Afya inatekeleza wajibu wake utadhani yeye ni daktari wa binadamu kumbe ni mwanasheria,” anamaliza kwa kusema Seif.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live